Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akihutubia madiwani wa Halmashauri hiyo
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa (aliyesimama), kulia kwake ni mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bi Pudensiana Kisaka na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela
Baadhi ya Madiwani wakiwa makini kumsikiliza mkuu wa Wilaya
Awali ya yote nimshukuru mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kujumuika pamoja nanyi leo hii. Pia niwashukuru kwa kunipa nafasi adimu niweze kuongea kwenye hadhara hii muhimu. Pamoja na muda kuwa mdogo niruhusuni niseme machache.
Kwanza kabisa niwapongeze kwa kuendelea kufanya kazi vizuri mara baada ya kuchaguliwa na kuapishwa kasi yenu ya kuleta maendeleo katika halmashauri imeonekana wazi na si ya kutilia shaka kwamba tutasonga mbele.
Kabla ya yote naomba nitangaze hali kuwa hali si nzuri katika halmashauri yetu ya Iringa kutokana na maafa na janga lililo tukumba. Katika tarafa ya Idodi kumetokea maafa ambapo mto Mapogoro umeacha njia na kuharibu nyumba pamoja na barabara. Kaya 75 zenye watu 377 zina hali mbaya sana wengi wao wakiwa hawana mahali pa kukaa na kitongoji chote cha Kitawena kinatakiwa kuhama. Barabara ya kwenda Msembe na Tungamalenga imekatika.
Nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri Mama Pudenciana Kisaka na timu yake yote walivyojitokeza kufanya kazi nzuri na kuhakikisha hali inakuwa shwari na hamna maisha ya mtu yanapotea. Pia nimpongeze Katibu tarafa Idodi Bwana Yakubu Kiwanga kwa kujitoa muhanga siku zote kuhangaika na wananchi akishikiana na watendaji na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wananchi wanusurika na madhara wote hawa wamefanya kazi katika mazingira magumu wakiwa hawana vitendea kazi kwa kweli wote Mungu aendelee kuwaimarisha katika utumishi wenu. Pia nimpongeze Mheshimiwa William Lukuvi (mbunge) kwa ukaribu wake na msaada mkubwa aliotoa.
Niwatoe hofu waeshimiwa madiwani nilifika eneo la tukio, pia kamati ya maafa ilifika eneo la tukio na tumefanya tathmini na kukubaliana kuwa wananchi wahame na wajengewe eneo lingine salama. Tayari mahema yamekwisha wekwa eneo jipya jana nimefika tena huko kujihakikishia na kaya 15 kati ya 75 zinalala kwenye mahema. Tayari tumepeleka maombi kwenye kamati ya maafa ya taifa kuomba msaada wa mabati ili tujenge nyumba za muda kwa wananchi waweze kuhamia.
Tunashukuru serikali imetoa tani 100 za chakula ambapo tani 7 zimekwisha gawanywa ambapo kijiji cha Idodi tani 2, kitisi tani 2 na mapogoro 3. Niaombe waheshimiwa madiwani tusadiane kusimamia chakula hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nitumie hadhara hii kushauri, tuache utaratibu wa kugawa mahindi ambao bado unamuongezea mhanga wa maafa gharama za kusaga. Uwezekano wa kusaga upo sijui kwa nini hatutaki kuutumia. Gharama za kusafirisha kutoka Makambako ni kubwa, Mimi kama Mwenyekiti wa Maafa naona ni bora tuka waambia Bodi ya nafaka yenye kinu kikubwa wakachukue mahindi hayo wasage, watupe sisi unga tuchukulie hapa hapa. Gharama za usafiri na kusaga tuwape wao hii itapunguza usumbufu wa kutafuta magari pia kutafuta wazabuni. Nimependekeza hili kwenye bodi ya nafaka naona wanalikubali wanalifanyia tathmini. Najua nitapata changamoto kwani wako waliokuwa wana nufaika na biashara hii ya kusafirisha mahindi na kuyagawa. Uzuri wake kwanza wananchi watapata unga, pili ugawaje utakuwa sio wa kupima kwa madebe kwani bodi itatufungia kwa kadri tunavyo taka. Naomba tuwafikirie wahanga kwanza tutafanikiwa.
Niruhusu pia nileze janga la kipindu pindu lililo tukumba katika tarafa ya Pawaga. Dalili zilianza kuonekana mnamo tarehe 7 katika kijiji cha Mbugani na Mboliboli. Mnamo tarehe 7/2/2016 majira ya saa 5 asubuhi kwenye mashamba ya umwagiliaji mfereji wa Kikeho kitongoji cha uwanja wa ndege A, Kijiji cha Mbugani Kata ya Mboliboli tarafa ya Pawaga, walijitokeza vibarua watatu waliokuwa wakiumwa homa ya matumbo kwenda kutibiwa hospitali ya Izazi daktari akashauri wabaki wanakotoka atapeleka huduma huko huko. Ilipofika jioni siku hiyo waliongezeka kufika 11 (Me 10, Ke 1). Ndipo ikaamuliwa kituo cha Afya cha St Lucas ndio kitumike kutibu wagonjwa wa kipindupindu (kipo kijij cha Mboliboli). Nimpongeze tena Mkurugenzi wa halmashauri na timu yake kwa kasi waliochukua kuhakikisha wanadhibiti ugonjwa usisambae. Kuna maamuzi ya dharura ambayo wamefanya ikiwemo kununua vifaa MSD naamini waheshimiwa madiwani mtaridhia matumizi hayo pindi yatakapoletwa kwenye vikao. Shukrani pia kwa mganga mkuu wa mkoa na wa wilaya pamoja na madaktari wote na wahudumu wa afya pamoja na madereva walihangaika usiku kucha kusafirisha vifaa kwa ajili ya zoezi hili. Wapo wengi wa kushukuru naomba tu wote mkubali shukrani zangu na Mungu azidi kuwapa maisha marefu muwatumikie wananchi.
Hali bado sio nzuri mpaka jana naondoka kwenye eneo la janga baada ya kuzungumza na wananchi takwimu zianonyesha kuna wagonjwa Hadi kufikia saa 1.30 usiku kituo kilipokea wagonjwa wapya 11 (Me 5, Ke6) Hivyo basi toka kambi ianze kituo kimehudumia wagonjwa 96 (Ke 26, Me 75), kati yao watoto chini ya miaka 5 ni 5 (Ke 2, Me 3). Mpaka sasa walio ruhusiwa 30, walibaki kituoni kwa matibabu 65 kati yake 8 hali yao ni nzuri wanaweza kuruhusiwa wakati wowote. Tunasikitika kupoteza mgonjwa mmoja kibarua ambaye alifika kituoni akiwa tayari mahututi huyu ni mwenyeji wa Kilolo na amezikwa kwa taratibu zote za kitabibu na sheria. Na Hali ya kituo kupokea wagonjwa ni tete. Tunaendelea kuwaomba msaada ikiwemo vifaa kama magodoro, neti, na mashuka kwa ajili ya wagonjwa.
Pia niwaombe madiwani wote watangaze hali ya hatari katika maeneo yao, marufuku kuuza vyakula ovyo, wananchi wanawe maji moto, wale vyakula vya moto. Wachemshe maji ya kunywa na ya kuoga kwani wengi hunywa maji pale wanapo oga. Pia marufuku kuoga mtoni kwa kipindi hiki au kwenye maji yaliyo tuama. Ukiona dalili za mgonjwa mkimbize kituo cha afya huku ukumpa maji mengi, ukimchelewesha mgonjwa dakika 45 au akaharisha mara 3 hali yake inaweza kubadilika kabisa. Nawa sana na sabuni. Ukifika hospitali usiondoke mpaka na wewe umepimwa au umejisafisha vya kutosha.
Mh Mwenyekiti
Kwa vile kikao hiki mimi ni mwalikwa tu naomba ruhusa niseme yale ambayo ningetamani yangefanyiwa kazi has baada ya kusoma kablasha nilipopewa kwa nilisoma kwa haraka haraka hivyo mtanisamehe kama nitasema ambalo limekwisha fanyiwa kazi.
Nianze na mfuko wa TASAF na utekelezaji wake;
Niombe kushauri waheshimiwa madiwani mtusaidie sana kuhakikisha hela hizi zinawafikia walengwa ningependa kuona taarifa za kamati za maendeleo za kata zinainisha watu walionufaika na mfuko huu, pia kuona watu hawajirudii kila mwaka kwani nia ni kumvusha kutoka kwenye lindi la umaskini aweze kujimudu. Pia niendelee kushauri kuunganisha utoaji wa fedha na kujiunga kwa CHF ili waweze kupata matibabu ingawaje angalizo kubwa liwe je eneo hilo lina kituo cha afya au zahanati? Kabla ya kuwachangisha walengwa.
Lakini nimeingiwa na hofu kubwa sana nilipo ona fedha nyingi imetumika kwenye ufuatiliaji (administrative cost) ipo haja ya kupunguza ziende kwa walengwa (21,079,500- usimamizi na ufuatiliaji ngazi ya Halmashauri, 14,051,181-ngazi ya kata na 119,450.499.90- Posho na nauli). Naomba kushauri tutafute njia nyepesi ya electroniki ambayo itapunguza gharama hizi. (Jumla karibu Tshs 154,581,180 fedha hizi ni karibu kaya 1000 maskini tungeweza kuzifikia fedha za usimazi haiwezakani zikaendelea kuwa 11% ya fedha tunazo pata kwa ajili ya maskini).
Afya
Kasi ya kuhamasisha kwa wananchi kujiunga na CHF ni ndogo mno ndio maana juhudi za ziada zainatakiwa kuhakikisha kwa pamoja waheshimiwa madiwani tunaongeza nguvu. Tujaribu kuhamasisha uza mahindi jiunge na huduma ya CHF kwa mwaka inawe kuwa debe 1 au mawili. Niombe waheshimiwa madiwani tusaidiane kwa hili. Sanjali na hili niwaombe waheshimiwa madiwani ujenzi wa vituo vya afya kwa zile kata ambazo bado kama inawezekana waalike vyombo vya dini au sekta binafsi ishiriki katika ujenzi. Nimpongeze Diwani wa Mseke ambaye ameniletea mchoro na BOQ za kituo cha afya nami naendelea kuomba omba wafadhiri mabalimbali ishallah mwenyezi Mungu atusaidie tupate wafadhiri. Lakini pia ni jukumu letu kila kijiji kuwa na zahanati. Tuhamasishe wananchi wakusanye mawe ya msingi baade tutaenda hatua ya pili. Muhimu tukaanza na kutenga jumamosi moja ya kukusanya mawe tu.
UKIMWI
Hali ya maambukizi ya UKIMWI bado ni changamoto kubwa kwa halmashauri. Nashauri tuanzishe mfuko wa ndani na kudunduliza kidogo kidogo kwani wahisani wameacha kuchangia kwenye bajeti kubwa ya serikali muhimu tukaanza mapema.
Lishe
Tumebahatika kutembelewa na Mkurugenzi Mkazi wa UNICEF wiki hii, amejionea hali halisi pia takwimu zisizolizisha za lishe duni. Kuna taarifa kuwa 51% ya watoto wetu wamedumaa jambo ambalo ni hatari sana. Naomba tusaidiane kwenye kuhamasisha chakula bora. Kila mtoto chini ya miaka 15 ale nyanya walau 1 kwa siku, au ale tunda pamoja na lishe bora. Pia tuhamasishe watumie virutubishi havina madhara yoyote. Wote tupande bustani ya mboga mboga kwa ajili ya chakula.
Rasimu ya Sheria Ndogo-Kodi ya Majengo
Hongera sana kwa kuleta rasimu hii naamini waheshimiwa madiwani wataridhia kwani imechelewa sana. Najua yapo mapendekezo niruhusu nishauri kwenye viwango; muhimu mkaangalia upya tozo zifuatazo;- Nyumba za kulala wageni (aidha iwe thamani ya jengo au kiwango cha mapato), Vituo vya mafuta (100,000 ni kiwango kidogo sana kwa mwaka), Hoteli na mahema ya kitalii 100, 000 ni ndogo sana naamini hata 1,000,000 bado ni ndogo). Upande wa Hospitali na zahanati hawa hata wakiwa exempted maana huduma yao inahitajika sana). Pia majengo yaliyopo kwenye maeneo ya uwekezaji yangepimwa kwa thamani ya jengo)
Taarifa ya fedha
Ombi langu kubwa ni kubuni vyanzo vipya vya ndani ili tuweze kumudu kasi ya maendelao. Kila Kamati ya kata ije na wazo lake tukae pamoja kujadili bila kudai posho ili tuibue vyanzo vipya. KAMAKA zote zilete mapendekezo.
Mwenyekiti naomba uniruhusu nishauri kwenye eneo la maombi ya kupunguza tozo la asilimia 30 kwa wanaoshindwa kurejesha mkopo. Ni muhimu kabla ya kuridhia pendekezo hili mkafanya tathmini ni kiasi gani kinatakiwa kusamehewa tusitoe “blanket” msamaha unaweza rudisha juhudi nyuma za wale walipaji wazuri. Pia lazima wanao samehewa wawe wale ambao hawakutumia vibaya fedha hizo.
Upande wa uwekezaji kwenye taasisi za fedha; ni muhimu kuangalia au kuwa na mshauri mapato (Treasury advisor) ambaye jukumu lake litakuwa kuangalia hasara na faida na kushauri haraka pale ambapo soko la hisa haliendi vizuri. Nashauri pia maelezo yatolewe kwa nini thamani ya hisa ya benki ya CRDB, UTT zimeshuka toka 2014 hadi 2015. Je 2016 baraza lako linashauriwa liendelee kuwekeza au litafute mahali pengine. Biashara hii ya amana ni ya masaa 24 kila siku sio ya kuweka kusubiri mwaka uishe.
Madeni; Nimeshtushwa na deni la 5,000,000, ingawaje sijui la muda gani lakini si vyema muendesha machinjio akadaiwa. Nilitaka kushauri kuboresha machinjio yetu ili kuhakisha hali ya usafi na yawe ya kisasa ili kukuza ufugaji wenye tija na kupata nyama bora. Pia sanjali na hili sikuona mapato yanayo tokana na samaki kama yapo ni madogo sana kulinganisha na uhalisia. Nilipo tembelea bwawa la Mtera wananchi walionyesha hofu kuwa mapato ya samaki hayafiki Halmashauri kwani aliyepewa kazi ya kukusanya huwakilisha kidogo sana. Ushauri wangu liangaliwe vizuri. (Nilipishana na fuso 3 siku 1)
Elimu
Pamoja na serikali kusaidia kuleta elimu bila malipo bado tuna changamoto kukamilisha madarasa pamoja na nyumba za walimu. Yapo madarasa ambayo hali yake si nzuri paa limeliwa na mchwa. Mazingira ya sasa na nyumba wanazo ishi walimu ni duni. Niombe kila Mheshimiwa Diwani afanye tathmini katika kata yake kujua ubora wa madarasa yanayotumika na nyumba za walimu.
Pia suala la madawati Mheshimiwa Rais Dr John Pombe Magufuli ametoa agizo kusiwepo tena na suala la mtoto kukaa chini. Kupitia KAMAKA ni muhimu tukatii agizo hili na kuanza utekelezaji wake mara moja. Upungufu ni madawati 9752. Nilitoa agizo kuwa mbao zote zinazo kamatwa halmashauri itumie kutengeneza madawati. Pia tuelekeze tozo la misitu na mkaa kwenye kuhakikisha madawati yanakamilika
Maji
Kuna changamoto nyingi hasa za miradi ambayo haijakamilika. Kata ya Ifunda, Mboliboli nimepokea malalamiko yao. Niliahidiwa na mhandisi wa maji ataniletea kablasha na maelezezo kwa kifupi kilichojili la mradi na wa maji Ifunda ili niunde Tume ya uchunguzi nasikitika sasa ni wiki ya 5 sijapata. Labda nikikuomba Mwenyekiti nitaweza kupata najua kwako inawezekana. Niliomba kwa nia njema tu.
Pia Mradi unaofadhiliwa na Mheshimiwa Dr Jakaya Kikwete Rais Mstaafu , Nyumba za watumishi wa jumuiya ya watumiaji maji ni muhimu Mh Kikwete akapelekewa taarifa ya maendeleo ya mradi huo na kumueleza hatua iliyofikia. Pia ni muhimu taarifa ya ‘liquidated damages’ ikajulikana ni kiasi gani cha fedha.
Ardhi
Nipongeze upimaji wa ardhi naomba pia nishauri umuhimu wa kutoa ramani elekezi kwa wale watakao pewa viwanja hivyo ili kuboresha makazi na kubadili sura ya eneo husika. Nipongeze juhudi za halmashauri katika kutatua migogoro.
Mgogoro wa Kata ya Ifunda ushughulikiwe haraka kwani unaendelea kujenga hamasa hasi bila sababu.
Mazingira
Iringa DC tunatakiwa tupande miti milioni 5 kwa mwaka huu. Tuhamasishe kila kata na kila taasisi ipande miti bila kuchoka. Pia tuwe mstari wa mbele kwa usafi.
Waheshimiwa madiwani naomba sana sula la ujenzi wa vyoo bora ni la muhimu sana tena sana. Mlipuko wa magonjwa utaendelea kutuandama tusipojenga vyoo. Tujiwekee malengo kuhamasisha jambo hili.
Kilimo
Zipo changamoto za hali ya hewa tuhamasishe kilimo cha mazao yanayo himili ukame kama Mtama. Pia mazao ya muda mfupi. Pia mazao mengi yamesombwa na maji ni muhimu tukashawishi wananchi wakapanda upya mazao. Tuhakikishe tunapata mbegu za viazi lishe na mihogo kupambana na hali hii.
Umwagiliaji umepata changamoto kwani uharibu wa miundo mbinu ya umwagiliaji ni mkubwa. Nashauri tuanze kufikiria miundo mbinu ya kisasa (drip irrigation) ili kukabiliana na hali hii.
Kuna maghala ambayo hayajamilika nni muhimu Mwenyekiti ukayatembelea na kujua tatizo liko wapi kwani mengine tumesaidiwa na wahisani na tunaweza poteza msaada.
Sekta ya ushirika
Mheshimiwa Mwenyekiti malalamiko ni mengi kwenye sekta hii ni muhimu yakatatuliwa haraka na wahusika wakapelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Maadili
Ni muhimu tukazingatia maadili. Ningependa kuona taarifa za watumishi wanaokiuka maadili. Si lazima wawe wa halmashauri, najua wako mahakimu, wako madaktari, wapo askari polisi n.k. waheshimiwa madiwani naomba taarifa zije. Mfano tunapoenda kwenye mikutano ya hadhara inakuwa aibu wananchi wanapolisema hadharani kumbe tungelipata mapema lisingefika huko.
Tulikuwa Itunundu wananchi walilalamika kuhusu askari magereza, Pawaga tulipata malalamiko ya Katibu tarafa (ambaye kwa mujibu wa ofisi ya RAS amesimamishwa hatakiwi kuudhuria vikao vya Baraza), Migoli nilipata malalamiko ya Hakimu. Naomba tuyaweke bayana kwani yanatokea kwa wananchi wenu na wengine mnayajua.
Mwisho kabisa lakini sio kwa umuhimu ni suala la waraka na barua ya serikali kwa Halmashuri ambayo imeonekana utekelezaji wake bado una changamoto hatari yake ni Mkurugenzi kuonekana ana kaidi melekezo ya serikali. Niwaombe waheshimiwa madiwani kama ombi hili linaonekana halifai ni muhimu mkaandika waraka na kuonyesha sababu za msingi kwa nini hamtaki makatibu tarafa wasishiriki vikao vya kamati zenu. Mimi ni mjumbe tu na mjumbe hauwawi yako yanasemwa kuwa inawekana hamtaki uwazi (transparency), Nia ya serikali ni kuhakikisha inasimamia fedha zake inazozitoa kwa halmashauri husika na makatibu tarafa ni wawakilishi halali wa serikali. Ninao waraka pamoja na barua toka kwa RAS unaosisitiza haya nisemayo. Mpaka sasa hatujapokea taarifa tofauti toka serikali kuu.
0 comments:
Post a Comment