Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha salim Jecha
Mgombea urais wa chama hicho, Said Soud alithibitisha kushiriki katika uchaguzi huo wakati alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, uchaguzi huo ndio utaratibu unaokubalika kwa mujibu wa Katiba wa kupata viongozi watakao ongoza dola.
Akifafanua ombi lake kwa Dk Magufuli, Soud alidai kuwa Pemba kumeanza kujitokeza viashiria vya vitendo vya vitisho vyenye kuhatarisha demokrasia, amani na utulivu. Alisema, Kamati Tendaji ya AFP imetathmini na kuamua kushiriki katika uchaguzi wa marudio, kwa sababu ule wa awali ulifutwa kwa mujibu wa sheria na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambayo ndio taasisi halali inayoshughulikia masuala yote ya uchaguzi.
Alisema, chama chake hakikuona sababu ya kususa uchaguzi huo wa marudio kwa sababu kufanya hivyo ni kuwanyima wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka katika kipindi cha miaka mitano, kwa ajili ya kuleta maendeleo.
“Chama cha Wakulima kimeamua kushiriki uchaguzi wa marudio uliotangazwa na ZEC kufuatia ule wa Oktoba 25, mwaka jana kufutwa kutokana na kasoro mbalimbali,” alisema. Alieleza kuwa, mandalizi ya uchaguzi huo kwa upande wa chama hicho yanaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na kuwapiga msasa viongozi watakaosimama kwenye majimbo ya uchaguzi kuwania uwakilishi na udiwani.
Aidha, Soud alimuomba Rais John Magufuli kuimarisha ulinzi katika kipindi cha harakati za kuelekea kwenye uchaguzi huo hasa katika kisiwa cha Pemba, kufuatia wananchi wengi kuamini kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika bila ya Chama cha Wananchi (CUF), hivyo kufikiria vurugu.
Alisema tayari kumejitokeza baadhi ya wananchi wanaowatia hofu wafuasi wa vyama vingine vilivyothibitisha kushiriki uchaguzi kwa kuweka alama X kwenye nyumba zao, pia kusambazwa kwa vipepeushi vyenye ujumbe unaoashiria uvunjifu wa amani.
Wakati ZEC ikiwa katika hatua za mwisho za kutangaza vyama vya siasa na wagombea wake watakaoshiriki katika uchaguzi wa marudio, jumla ya vyama sita vimethibitisha ushiriki wao kwa kuandika barua kwenda ZEC. Vyama hivyo ni CCK, SAU, TLP, CCM, TADEA na AFP.
0 comments:
Post a Comment