METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 17, 2015

Magari yanayozidisha uzito yageuzwa mradi wa barabara


Kumekuwa na tuhuma kwamba usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya Reli ya Kati na Tazara umekuwa ukihujumiwa kwa makusudi ili wamiliki binafsi wa malori na mabasi wachume fedha kwa kufanya biashara hiyo.
Matokeo yake ni uharibifu wa barabara na miundombinu mingine, huku wananchi wakiteseka kwa kukosa huduma ya vyombo vya usafirishaji vyenye unafuu na uhakika.
Bado kila siku inashuhudiwa magari makubwa ya kubebea mizigo na abiria yakiwa yamejaza kupita kiasi, huku ikifahamika kwamba pindi yanapopita kwenye barabara ni lazima kutatokea uharibifu wa miundombinu hiyo.
Ni vyema kupita kwenye barabara zenye lami, kwani safari yako inakuwa na uhakika wa kufika salama, lakini inaweza kugeuka shubiri pale utakapokutana na barabara mbovu.
Inafahamika kwamba ujazo wa magari kupita kiasi pia ni sababu ya uharibifu wa barabara nchini.
Kwa kuyatoza ushuru wa petroli, magari ya kigeni na yanayozidisha uzito kwenye mizani, Mfuko wa Barabara(RF),  umekusanya Sh293 bilioni.
Meneja mfuko huo, Joseph Haule anasema upatikanaji wa ushuru huo kupitia vyanzo hivyo vitatu umesaidia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
Anasema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, asilimia mbili ya mapato yote yalitokana na tozo ya magari yanayozidisha uzito na kuongeza kuwa lengo ni kudhibiti magari ya mizigo na abiria yasizidishe uzito.
“Tozo hii hukusanywa kwenye vituo vya mizani pale inapobainika kuwa gari limezidisha uzito kinyume cha sheria,’’ anasema Haule
Anaeleza kwamba uzidishaji wa uzito ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa barabara nchini na kwamba kiwango hicho cha tozo hakiwezi kufidia uharibifu unaofanywa na magari husika.
Haule anasema siku wafanyabiashara watakapotimiza wajibu wao wa kutokuzidisha uzito, kiwango hicho kitafutika na hakitachangia kitu chochote kwenye mfuko huo.
Anasema  tozo ya mafuta ni chanzo kikuu cha mapato ya mfuko ambacho huchangia asilimia 97 ya mapato yote ya mfuko huo na kupitia chanzo hicho, watumiaji wa barabara huchangia Sh263 kwa kila lita ya petroli au dizeli wanayonunua. Kuhusu  tozo ya magari ya kigeni mipakani, Haule anasema yanachangia kwa asilimia moja  kwenye mfuko  huo, kwani kiwango kinachotozwa ni Dola 16 za Marekani sawa na Sh33,600 kwa kilomita 100.
“Mchango wa chanzo hiki unategemea ubora wa barabara zetu na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam kuvutia wafanyabiashara wa nchi za jirani kutumia miundombinu hiyo kusafirishia mizigo,’’ anasema.
Meneja msaidizi wa mfuko huo, Ronald Lwakatare anasema baada ya kukusanya ushuru huo wa Sh2,931 bilioni, fedha hizo ziligawanywa kwenye idara husika zikiwamo Wakala wa Barabara  (Tanroads) iliyopatiwa Sh1,829 bilioni, Ofisi ya Waziri na Mkuu (Tamisemi) Sh 874 bilioni na Wizara ya Ujenzi Sh200 bilioni na mfuko huo ukabakiwa na 27.33 bilioni.
Lwakatare anasema barabara isipofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, huharibika  kidogo kidogo.
Anasema: “Utafiti uliofanywa Afrika Kusini na shirika la ‘The South African National Road Agency,’ unaonyesha kuwa kama uharibifu  mdogo usipofanyiwa matengenezo kuna uwezekano wa barabara yote kuharibika kabisa na kuhitajika kujengwa upya.’’
Anafafanua kuwa ikiwa matengenezo yatafanywa baada ya miaka mitatu tangu uharibifu utokee, gharamaza matengenezo hupanda mara sita zaidi na mara 18 ikiwa matengenezo hayatafanywa katika miaka mitano.
Lwakatare anasema ubora wa hali ya barabara huchangia kupanda au kushuka kwa kiwango cha nauli kinachotozwa kwa abiria na mizigo, pia muda unaotumika kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Idadi ya magari yanayotoa huduma katika njia yoyote hutegemea ubora wa barabara,” anasema.
Utafiti uliofanywa mwaka 2006 na Tanroads kwa pamoja na Jumuiya ya Ulaya kupitia mradi wa Rusrim ulibaini kuwa gharama ya nauli kati ya Mbamba Bay na Songea Mjini ilishuka kutoka 10,000 hadi 5,000 baada ya matengenezo ya barabara kukamilika.
Anasema kutokana na mtandao wa barabara kufanyiwa matengenezo mara kwa mara, nchi jirani za Malawi, Zambia, Burundi, DRC, Rwanda na Uganda hutumia barabara za Tanzania kwa kupitisha mizigo Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kuchangia kuinua uchumi wa Taifa.
Amesema Bodi ya Barabara ilifanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na matokeo yake yametumika kuishauri Serikali namna ya kuziba mianya ya ukwepaji kodi ikiwamo suala la uchakachuaji na uuzaji wa mafuta ambayo hayajalipiwa kodi kutoka nchi jirani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com