METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 3, 2015

MAONI: Ni janga wahitimu 18,000 kutupwa mitaani

 

Ni wakati mwingine wa vilio kwikwi na majonzi kwa wazazi, walezi na hata wanafunzi zaidi ya 18,000 waliokosa nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha tano kwenye shule za sekondari za umma mwaka huu.
Kwa hakika, hizi si habari njema tunapoona watoto 18,751 tena wenye sifa ya kujiunga na masomo ya kidato cha tano, wakiikosa, eti kwa sababu mbalimbali.
Tumetajiwa sababu hizo kuwa ni pamoja na baadhi yao kukosa sifa kwa sababu au kigezo cha umri mkubwa na wengine kuwa watahiniwa wa kujitegemea. Tunajiuliza, je, watahiniwa binafsi hawapaswi kujiendeleza kwa kupatiwa nafasi kwenye shule za Serikali kama sehemu ya kujali juhudi zao, wazazi au wale waliojinyima fedha zao nyingi ili kuhakikisha wanafikia elimu ya kidato cha nne?
Sababu hizo zinawezwa kuitwa za kibaguzi, hazifai kuachwa ziendelee katika nchi yetu, badala yake tunashauri wizara zinazohusika na usimamizi wa elimu, yaani Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Elimu na Mafunzo ya Ufundi zishirikiane ili zihakikishe mfumo huu wa kibaguzi wa kuwanyima wanafunzi nafasi kwa sababu ya umri, unaondolewa.
Tunaamini, Serikali inaweza kuwa haitaki kusema ukweli, zipo sababu zaidi za vijana wetu kukosa nafasi za kidato cha tano, zikiwamo za kutokuwapo kwa nafasi za kutosha za madarasa, mabweni kwenye shule za umma, ukosefu wa uwezo wa kuwalisha wanafunzi wote, hasa wa shule za bweni, kwani malipo ya wazabuni kwenye taasisi za umma yamekuwa tatizo.
Pamoja na kuambiwa na Serikali kuhusu ongezeko la ufaulu kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana na kupata nafasi zaidi ya 900 ikilinganishwa na zile za mwaka jana, bado tunajiuliza, ilijiandaa vipi katika  kuhakikisha wote waliofaulu wanapata fursa ya kuingia kidato cha tano?
Tunaiamini Serikali tangu ile ya Awamu ya Tatu ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa iliyoasisi Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) na hatimaye ule wa elimu ya sekondari (MMES), iliyoendelea kutelekezwa wakati huu wa awamu ya nne,  ingawa kwa jina jipya, Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Hata hivyo, tunajiuliza, uko wapi umakini wa Serikali wakati huu inapotekeleza BRN? Je, imehakikishia vipi kwamba wanafunzi wote wanaofaulu mitihani yao kwa ngazi mbalimbali wanapata nafasi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu?
 Hilo lilitokea mwaka jana kwa wahitimu wa darasa la saba, wapo waliachwa, wametulia mitaani bila stadi au ujuzi, hawana uwezo wala nyenzo ya kujitegemea, baadhi yao umri wao ukiwa mdogo. Je, ni nani anayewajali watoto hawa walioingizwa kwenye soko katili la ajira lisilo na huruma washindane na wahitimu wengine wakiwamo wa vyuo vikuu, ambao pia hawana ajira?
Serikali ituambie kwa nini ilihimiza ujenzi, ufunguzi wa shule za sekondari za kata, ikaajiri walimu wote waliohitimu vyuo, ambao wamefanya kazi nzuri ya kufundisha watoto wetu wakafaulu, ilifikiria nini kuhusu wahitimu hao baada ya kidato cha nne?
Tunadhani ilipaswa kuangalia mahitaji ya kidato cha tano na sita kwa kuhakikisha kuwa kila kata yenye shule za kidato cha kwanza hadi cha nne, inajengwa moja ya kidato cha tano na sita. Vinginevyo, tukae  tusubiri janga jipya la wahitimu wa kidato cha sita kukosa nafasi kwenye vyuo vikuu nchini. Tunakwenda wapi?
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com