METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 14, 2015

Majambazi waua 7 kituo cha Polisi

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu akizungumza na waandishi wa habari alipowasili kukagua Kituo cha Polisi Sitaki Shari Ukonga, Dar es Salaam jana baada ya kuvamiwa na majambazi wanaodaiwa kupora silaha kituoni hapo juzi usiku. Askari wanne na raia watatu waliuawa katika tukio hilo. Kulia kwake ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova. (Na Mpigapicha Wetu).
ASKARI wanne na raia watatu wameuawa baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kuvamia Kituo cha Polisi cha Sitakishari kilichopo Ukonga katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana baada ya majambazi kufika kituoni hapo saa tano usiku kama wananchi wanaohitaji huduma kituoni hapo, lakini baada ya kuhojiwa na askari waliokuwa zamu waliwafyatulia risasi askari hao na kuwaua wanne.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu, akithibitisha alisema miongoni mwa raia waliouawa ni mmoja wa waliofika kituoni hapo akiwa ameongozana na majambazi waliotekeleza tukio hilo la kutisha.
“Inasemekana kundi hili la majambazi lilifika kama wananchi wanaohitaji huduma, lakini walipoonekana tofauti na raia wema wakaulizwa nini wanahitaji kusaidiwa, ndipo waliwafyatulia risasi na kuwaua askari waliokuwepo hapo na kuendelea kuelekea ndani ya kituo,” alisema Mangu.
Alisema katika 'fyatua fyatua’ hiyo ya risasi, majambazi hao waliwaua askari wanne papo hapo na raia watatu. IGP Mangu alisema baada ya kufanya mauaji hayo katika tukio linalotajwa kudumu kwa takribani dakika 45, kabla ya kuzimwa na polisi, majambazi hao walipora silaha ambazo zilikuwepo kituoni hapo na idadi yake haijajulikana hadi hapo utafiti utakapokamilika.
“Uharibifu mkubwa umetokea ikiwemo wizi wa silaha ambazo hadi hivi sasa idadi yake haijajulikana hadi utafiti ukamilike,’’ alisema. Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadick alisema wananchi wasiwe na hofu kwani usalama wao unalindwa na kikubwa watoe ushirikiano kwa polisi ili kuweza kuwabaini wahalifu hao.
“Tukio hili ni la kusikitisha sana ambalo limepoteza uhai wa askari wetu pamoja na wananchi. Kila mtu anapaswa kulikemea na kutoa ushirikiano ili tuweze kuwabaini hawa waliotenda tukio hili kwani nina imani wanaishi ndani ya jamii yetu na tunawafahamu,” alisema Sadick.
Alisema wahalifu hawa wanatumia usafiri ambao unajulikana kwa wananchi, wanaishi na kufanya mambo mengi ndani ya jamii; hivyo wananchi wasiache kutoa taarifa mahali walipo ili kufanikisha kukamatwa kwao na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema saa tano usiku walisikia milio ya risasi kituoni hapo na kudhani kuwa watuhumiwa wametoroka na kwamba polisi wanafanya juhudi za kuwarudisha, lakini hali ikawa sio shwari baada ya milio ya risasi kuongezeka.
“Tulikuwa tumekaa hapa nje, mara tukasikia mlio wa risasi kisha ikaendelea kwa kasi, tukakimbilia ndani na kujifungia maana tukio la milio ya risasi lilichukua muda mrefu sana kama saa moja hivi,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyepo jirani na kituo hicho ambaye hakupenda jina lake liandikwe.
Kutokea kwa tukio hili la uvamizi katika kituo cha polisi ni mwendelezo wa uvamizi ambao umekuwa ukitokea mara kwa mara vituo vya polisi kuvamiwa na watu wenye lengo la kupora silaha na kuwaua askari wanaowakuta ndani ya vituo hivyo
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com