METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 26, 2015

Wahadzabe hawamwamini mtu

Mzee Maidona Wazael kutoka jamii ya Wahdzabe akiwa mbele ya nyumba yake

AMAYEGAAMO na Mdana Amayegama Ama ni salamu inayotumiwa na watu wa jamii ya Wahadzabe ikiwa ni salamu ya jumla.

Sehemu kubwa ya jamii hiyo bado inaishi katika maisha ya ujima, chakula chao kikuu ni nyama, mizizi, matunda na asali. Pia jamii hiyo inaendelea kuishi kwenye viota katikati ya pori. Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone inaonesha juhudi nyingi zinafanyika katika kusaidia jamii hiyo.


Wahadzabe ni miongoni mwa makabila madogo zaidi sana linalopatikana kaskazini mwa Tanzania kando ya ziwa Eyasi kwenye bonde la ufa na kupakana na uwanda wa Serengeti pia wamekuwa wakipatikana katika wilaya ya Mkalama mkoani Singida. Jamii hiyo inatajwa kuwa ni ya mwisho kabisa barani Afrika inayotegemea uwindaji na ukusanyaji kwa ajili ya kuishi.

Wahadzabe wapo katika hatari ya kupoteza asili yao kwa kuwa maeneo waliyokuwa wakiishi tangu enzi za mababu yamevamiwa na wakulima na wafugaji. Dk Kone anasema, jamii hiyo inabadilika taratibu na ukiwa unaenda nao kwa kasi wanaweza kukimbia. “Ila wana tabia moja huwa hawamwamini mtu,” anasema.

Kiongozi huyo anasema, mara ya kwanza alipopata wazo la kusaidia jamii hiyo wilayani Mkalama mkoani Singida aliwapelekea majembe 70 wayatumie kulima. Kwa mujibu wa Dk Kone, aliporudi huko kufuatilia matokeo ya zana hizo za kilimo akakuta wametumia mipini ya majembe hayo kwa kutengeneza visu na mikuki kwa ajili ya kuwindia.

Awamu ya pili akapeleka majembe 150 na hali haikuwa tofauti sana na hiyo. Hata walipopatiwa shamba la kulima lenye ukubwa wa ekari 10 baada ya kupanda hawakurudi tena kuangalia vimeota ana la na ulipofika msimu wa mavuno waliambulia gunia moja tu la mahindi.

Wakati wa sensa ya watu na makazi nchini mwaka 2012 hawakujitokeza ili wahesabiwe hivyo ikabidi kutafutwa kwa mbinu mbadala kufanikisha jambo hilo muhimu kwa taifa. Mbinu hiyo ilikuwa ni kuchinjwa kwa swala, nyama ikachomwa, wakaenda kwa wingi kutoka mafichoni walipokuwa.

Dk Kone anasema jamii hiyo inaanza kubadilika taratibu na hata baada ya watoto wao kupelekwa shule ya bweni ya Munguli kumeanza kuonekana mabadiliko kwenye jamii hiyo. Anasema madhumuni ya kujenga shule hiyo ya bweni maalum kwa ajili ya watoto wa kabila la Kihadzabe ni kuliendeleza kabila hilo linaloishi maisha ya porini ambayo kwa sasa hayakubaliki.

Dk Kone anasema, jamii ya Kihadzabe bado inaishi katika mazingira magumu ya kijima , chakula chao kikuu ni mizizi ya miti, asali, matunda pori, nyama ya wanyama pori na magome ya miti. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama, Bravo Lyapembile, anasema halmashauri hiyo ina mikakati ya kuendeleza watoto wa jamii hiyo.

Anasema hata ujenzi wa shule ya bweni ni sehemu ya mikakati hiyo kuwaendeleza Wahadzabe ili waishi maisha ya wakati uliopo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto hao baadaye wanakwenda kuibadilisha jamii hiyo kutokana na elimu waliyoipata.

Wakizungumza hivi karibuni wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa aliyetembelea kijiji cha Mungulu wanakoishi jamii hiyo, Mwenyekiti wa jamii ya Wahdzabe , Edward Mashimba anaiomba Serikali kuitengeneza barabara wanayopita.

Anasema barabara wanayotumia imekuwa na mashimo mengi na pia hakuna mtandao wa simu hali inayofanya wakose mawasiliano. “Kama serikali imeamua kubadilisha jamii hii basi tutengenezewe barabara na tupate mtandao wa simu,” anasema. Mashimba anasema, baadhi ya Wahadzabe wameanza kuhama porini na kuishi maisha ya kawaida na wengine wanaishi kijiji cha Munguli.

“Wahadzabe wanaoishi porini sasa ni wachache wengi walikubali kubadilika” anasema. Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Munguli, Daud Yohana anasema, Wahadzabe wanahitaji hifadhi ya msitu ili waweze kupata kitoweo cha nyama kwa kuwa kukiwa na msitu wanyama wataishi hapo. “Serikali ifikirie kutupatia msitu wa hifadhi ili tupate mahali pa kuwinda, tuwe na kitoweo kutokana na wanyama wengi kukimbilia mbali,” anasema.
Mzee wa Kihadzabe, Maidoma Wazael anasema, sasa jamii hiyo inakabiliwa na njaa kwa sababu msimu wa kilimo ulikuwa na mvua chache. ‘‘Mwaka huu mvua ni chache na bila mvua hakuna chakula kuna njaa hapa,” anasema. Wazael anasema, hata asali imekosekana kutokana na uhaba wa mvua na barabara ya kwenda eneo la Kipamba ni mbovu sana.

Kwa mujibu wa mzee huyo, juhudi za serikali za kuitaka jamii hiyo kubadilika zinaonekana kwani hata watoto waliokuwa wakiishi porini na wazazi wao waliondolewa na sasa wamepelekwa kusoma shule ya bweni ya Munguli. Anasema, kuna mabadiliko kwa jamii hiyo kwa sababu wanaanza kuishi maisha ya kawaida na wengi wao wamehama maporini na kuishi kijijini na familia zao huku wakiruhusu watoto wao waende shule.

Hata hivyo anasema bado kuna wazazi wanaoishi porini na watoto wao, hivyo juhudi zinafanyika ili kuwashawishi waende kuishi maisha ya kawaida.

“Tunataka jamii hii ibadilike, mwaka huu nilikwenda Dodoma pamoja na wenzangu kwenye wiki ya elimu na tulionesha ni kwa jinsi gani jamii inabadilika kwani watoto wa Kihadzabe waliotolewa porini na kupelekwa shule ya Munguli sasa wanajua kusoma na kuandika,” anasema.

Naibu Waziri Majaliwa anasema, hakuna anayeruhusiwa kufanya shughuli kwenye hifadhi kwani kuna maeneo yametengwa kwa ajili ya wafugaji na wakulima tu. Anamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama kupanga matumizi bora ya ardhi.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, serikali ina akiba kubwa ya chakula na hakuna Mtanzania atakayekufa kwa kukosa chakula. Anasema tayari waliagiza mikoa yote na halmashauri zote kufanya tathmini ya hali ya chakula ili wananchi wapelekewe chakula cha bei nafuu.

Majaliwa anawaeleza Wahadzabe kuwa, serikali imezungumza na kampuni ya simu ya Viatel ambayo inaleta teknolojia mpya ya simu ambapo mtandao huo utahudumia zaidi wananchi wa vijijini. Anawataka kubadilika na kuishi katika mazingira ya kawaida na amewahimiza kuhakikisha watoto wao wanakwenda shuleni.

CREDIT: HABARI LEO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com