MKURUGENZI
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amesema
kuwa urasimu mkubwa uliopo katika kusimamia masuala ya uwekekezaji umechangia
kuwakimbiza wawekezaji.
Alisema
hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza katika Baraza la Biashara la Mkoa wa
Kigoma. Alisema uchunguzi uliofanywa na taasisi yake umebaini Tanzania
inapoteza fursa nyingi za uwekezaji kutoka nje ya nchi kutokana na mazingira ya
urasimu na rushwa.
Simbeye
alisema kuwa urasimu huo pia umekuwa ukilalamikiwa na Mabalozi wanaoiwakilisha
nchi katika nchi mbalimbali ulimwengu ambao licha ya uhamasishaji mkubwa
wanaoufanya, wameishia kupata lawama kutoka kwa wawekezaji waliofika Tanzania
kutokana na urasimu waliokumbana nao.
Kutokana
na hali hiyo, Simbeye alisema Tanzania imepoteza fursa nyingi za uwekezaji
ambazo zingesaidia kukuza uchumi wa nchi kutoka hapa tulipo na kwamba Serikali
inapaswa ichukue hatua madhubuti katika kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mazingira ya Biashara kutoka Baraza la Taifa la Biashara nchini
(TNBC), Arthur Mtafya alisema kuwa utititri wa kodi na tatizo la upatikanaji wa
ardhi ni kikwazo kikubwa katika kuvutia wawekezaji nchini.
Mtafya
alisema masuala hayo na urasimu wa vituo vya usimamizi wa masuala ya uwekezaji
nchini, yanapaswa kuondolewa haraka ili kuweka mazingira ya kuvutia kwa
uwekezaji na ufanyaji biashara usio na usumbufu ambao utawezesha kuinua uchumi
wa nchi.
Akizungumza
katika baraza hilo Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Mwanga mjini
Kigoma, Raymond Ndabiyagese alisema kuwa kuwepo kwa Baraza la Biashara la Mkoa
kutasaidia kuwaweka pamoja wafanyabiashara, serikali na taasisi mbalimbali
zinazosimamia biashara ili kuzungumzia changamoto zinazowakabili
wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.
Awali
akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya aliwataka wakuu wa
wilaya za mkoa huo kuhakikisha mabaraza ya biashara katika wilaya zao
yanafanyika ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili kulingana na
mazingira yanayowazunguka huku akibainisha umuhimu wa kuwepo kwa mabaraza ya
biashara ya wilaya na mkoa kwa uchumi wa maeneo yao na taifa kwa jumla.
0 comments:
Post a Comment