METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, April 24, 2015

Baadhi ya machinjio jijini Dar es Salaam hayakidhi vigezo




Na Victor Mariki – Ofisi ya Makamu wa Rais

Baadhi ya machinjio jijini Dar es Salaam hayakidhi vigezo vya mazingira ya machinjio, hali ambayo huatarisha afya za wakazi wanaozunguka maeneo hayo ikiwemo pamoja na wafanyakazi machinjioni humo.

Hayo yalibainika wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu ya Rais - Mazingira, Mh. Binilith Mahenge alipofanya ziara ya ukaguzi mazingira katika baadhi ya machinjio hayo jijini humo leo.

Katika ziara hiyo, Mh. Mahenge alitembelea machinjio ya Ukonga na kubaini kuwa, machinjio hayo hayajakidhi vigezo vya mazingira ya machinjio ambavyo ni kuwepo kwa mabwawa maalum ya kuhifadhi majitaka yatokanayo na shughuli hizo ikiwemo na kusakafiwa kwa saruji eneo hilo.

 
Ilihali machinjio hayo huchinja ng'ombe 200 hadi 250 kwa siku ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala hutoza ushuru wa shilingi 2500 kwa kila ng'ombe na mmiliki wa machinjio hayo hutoza shilingi elfu 2 kwa kila ng'ombe kama gharama za uendeshaji shughuli hiyo.

Aidha Mh. Mahenge, alimtaka mmiliki wa machinjio hayo kutekeleza vigezo hivyo vya mazingira kwa kuwa suala hilo linaweza kufanyika kupitia mapato yatokanayo na shughuli za uendeshaji wa machinjio hayo.

Wakati huo huo pia, alitembelea machinjio ya Vingunguti ambapo Taarifa ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilieleza kuwa mazingira ya machinjio hayo hayaridhishi kutokana na uchakavu wa miundombinu yake.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa miundombinu iliyopo bado inaendeleza mfumo wa kizamani katika uendeshaji wa shughuli hizo hivyo kupelekea usafi wa maeneo hayo kuwa mgumu na usiokidhi vigezo vya mazingira.

Kufuatiwa Taarifa hiyo ya Halmashauri, Mh. Waziri alishauri na kuutaka uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuweka bajeti maalum ya kutunza na kuboresha mazingira ya machinjio hayo
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com