METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 18, 2025

REA YAENDELEA KUSAMBAZA MITUNGI YA GESI 16,275 MKOANI SIMIYU







WazoHuru - Simiyu

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Kihongosi, leo tarehe 18 Februari, 2025 amezindua rasmi zoezi la usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 katika mkoa wa Simiyu na kutoa wito kwa Wananchi kuchangamkia fursa ya matumizi ya nishati safi kama njia mbadala ya kupunguza uharibifu wa mazingira, uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Mhe. Kenani amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kulinda afya za Watanzania pamoja na kutunza mazingira ambapo amewahamasisha Wananchi wa mkoa wa Simiyu kununua mitungi hiyo ya gesi pamoja na vifaa vyake; mitungi inayosambazwa na kampuni ya ORYX Gas.

“Utekelezaji wa Mradi huu, unaunga mkono Mpango Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo, lengo ni kuhakikisha kuwa angalau asilimia 80 ya Watanzania, wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.” Amesema Mhe. Kihongosi.

Usambazaji wa mitungi hiyo ya gesi unatekelezwa kwa pamoja kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited, ambapo Wananchi wanapata fursa ya kukunua mitungi hiyo gesi ya kilo 6 kwa shilingi (20,000); bei ya ruzuku na kiasi kilichobaki kitalipwa na Serikali kupitia REA.

Naye Mhandisi wa Miradi ya Nishati Safi kutoka REA, Geofrey Gedo amesema Serikali, imedhamiria kuhakikisha Wanachi waliopo katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetenga fedha, takribani shilingi za Kitanzania milioni 325 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya kuhamasisha matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) kwa mkoa wa Simiyu.

“Mradi pia, unalenga katika kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti,ambapo takribani hekta laki 4 (400,000) hukatwa kila mwaka; wakati asilimia 63.5 ya kaya hutumia kuni kama chanzo kikuu cha nishati na asilimia 26.2 hutumia mkaa.

Mhandisi, Gedo ameongeza kuwa mitungi 16,275 itauzwa kwa bei ya punguzo ya asilimia 50 ambayo ni shilingi 20,000 katika mkoa wa Simiyu na kila wilaya ipata mitungi 3,255.

Wilaya za mkoa Simiyu zitakazonufaika na usambazaji huo ni pamoja na wilaya ya Maswa, Bariadi, Itilima, Meatu na Busega.

Mhandisi, Gedo ameongeza kuwa ili Wananchi wapate mitungi hiyo wanatakiwa kuwa na Kitambulisho cha NIDA pamoja na shilingi (20,000) na watakapofika katika vituo vya kuuzia mitungi hiyo wataulizwa majina yao, jinsia; namba ya nida; mkoa, wilaya, kata, kijiji na kitongoji /mtaa anapoishi.

“Natoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha zoezi hili na baada ya kununua mitungi hii; wanunue na kuendelea kutumia nishati ya gesi.

Share:

Saturday, November 30, 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Aahidi Kutatua Changamoto za Tanganyika Farmers Association (TFA) ili Kuongeza Faida kwa Wakulima













Leo, Novemba 30, 2024, Arusha ilikua jiji lenye hafla muhimu kwa wakulima wa Mkoa wa Arusha na maeneo mengine ya Tanzania. Ambapo mkutano mkuu wa wanahisa wa Tanganyika Farmers Association (TFA) ulifanyika katika viwanja vya Shopping Mall, ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Ndug. Gerald Mweli, alikua mgeni rasmi na alitoa ahadi ya kutatua changamoto zinazokikabili chama hicho, ili kuleta manufaa kwa wakulima.


Katika hotuba yake, Katibu Mkuu Mweli alieleza kuwa serikali inatambua mchango wa TFA katika kuunganisha wakulima na kutoa huduma muhimu kama vile ushauri wa kilimo na pembejeo. ambapo alikiri pia kwamba kuna changamoto ambazo wamezipeleka kwake kama vile riba kubwa kutoka kwa mabenki, ubora pembejeo, na ukosefu wa huduma za ugani. Aliahidi kushirikiana na TFA ili kutatua changamoto hizi na kuhakikisha wakulima wanapata fursa zaidi za kunufaika na huduma za chama hicho.


Mweli alisisitiza kwamba ushirikiano kati ya TFA na serikali ni muhimu ili kuimarisha uzalishaji wa wakulima na kuongeza tija katika kilimo. Aliwapongeza viongozi wa TFA kwa juhudi zao za kuboresha maisha ya wakulima na kuongeza uzalishaji kupitia kilimo cha kisasa.


Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TFA, Ndugu Waziri Barnaba, alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama wake ili kukuza uchumi wao kupitia kilimo. Mkurugenzi Mtendaji wa TFA, Jastin Shirima, aliongeza kuwa chama hicho kitatumia ushirikiano na serikali kuhakikisha wanachama wanapata mbolea za ruzuku kupitia matawi ya TFA yaliyo kote nchini.


Hii ni ahadi muhimu kwa wakulima wa Tanzania, na inatoa matumaini ya mafanikio zaidi kwa sekta ya kilimo mkutano huo ulihudhuriwa na Wanachama zaidi ya 500 kutoka Maeneo mbalimbali hapa nchini

Share:

Tuesday, October 22, 2024

GEITA YAUPOKEA MRADI WA BILIONI 17 KWA AJILI YA KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI 105

Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela akiongea na Wanahabari mara baada ya kumpokea rasmi mkandarasi, kampuni ya CCC (Beijing) Industrial & Commercial Ltd; kutoka China
Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, leo jioni, tarehe 22 Oktoba, 2024 akiongea na Wanahabari mara baada ya kumpokea rasmi mkandarasi, kampuni ya CCC (Beijing) Industrial & Commercial Ltd; kampuni kutoka China, iliyoshinda kandarasi ya Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye vitongoji 105 vya majimbo saba (7) ya mkoa wa Geita; Mradi utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili, kuanzia sasa.                           

Msimamizi wa Miradi ya REA mkoa wa Geita, Mhandisi, Dominick Mnaa akitoa taarifa ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali katika mkoa wa Geita mbela ya Mkuu huo wakati wa hafla hiyo, leo jioni, tarehe 22 Oktoba, 2024
Mwakilishi wa kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd, Bi. Carol Wang sambamba na Watumishi wengine wa kampuni hiyo wakimsikiliza Mhe. Martine Shigela, Mkuu wa mkoa wa Geita wakati wa hafla hiyo
Mwakilishi wa kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd, Bi. Carol Wang akitoa maelezo namna kapuni yake itakavyaotekeleza Mradi huo wa  kusambaza umeme kwenye vitongoji 105 vya mkoa wa Geita mbele ya Wanahabari
Msimamizi wa Miradi ya REA mkoa wa Geita, Mhandisi, Dominick Mnaa akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa vitongoji katika mkoa wa Geita kulia kwake ni Mhasibu Mwandamizi kutoka REA Bi. Innocencia Makinge wakati wa hafla hiyo, leo jioni, tarehe 22 Oktoba, 2024

Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, leo jioni, tarehe 22 Oktoba, 2024 amempokea rasmi, mkandarasi, kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd; kampuni kutoka China, iliyoshinda kandarasi ya Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye vitongoji 105 vya majimbo saba (7) ya mkoa wa Geita; Mradi utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili, kuanzia sasa. 

Mhe. Shigela amesema Geita imefungua ukurasa mpya wa upatikanaji wa nishati ya uhakika vijijini na kuongeza kuwa umeme utaenda kuongeza idadi ya vitongoji zaidi ya 105 na kuongeza kuwa Mradi huo, utazinufaisha pia sekta ya viwanda vidogo, madini, kilimo na uvuvi ambazo zimeajiri idadi kubwa ya watu mkoani Geita. 

“Nafarijika sana kuona namna REA walivyojipanga vizuri na kuja kumtambulisha mkandarasi ili aanze kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vya mkoa wetu”. 

“Mkoa wa Geita una jumla ya vijiji 486 ambapo kati ya hivyo vijiji 483 vimefikiwa na huduma ya umeme kupitia Miradi ya awali inayotekelezwa na REA na kuna vitongoji 2,195, huku vitongoji 1,017 vimekwishafikiwa na huduma ya umeme, kukamilika kwa Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 105 kwenye majimbo saba (7) ya mkoa wetu, kutaongeza upatikanaji wa nishati ya umeme”. Amekaririwa Mhe. Shigela. 

Katika taarifa yake ya awali; Msimamizi wa Miradi ya REA mkoa wa Geita, Mhandisi, Dominick Mnaa amemwambia Mkuu wa mkoa wa Geita kuwa, Mkoa una jumla ya kata 122, vijiji 486 na vitongoji 2,195, ambapo hadi sasa jumla ya kata 121, vijiji 483 na vitongoji 1,017 vimekwishafikiwa na huduma ya umeme. 

“Kata moja ya Izumacheli yenye vijiji vitatu (3) vya Izumacheli, Butwa na Lunazi bado havijafikiwa na huduma ya umeme, sababu za kutofikiwa na huduma ya umeme kwa kuwa vipo katika ziwa Viktoria hivyo basi Wakala wa Nishati Vijijin upo kwenye hatua za mwisho kutafuta mkandarasi kwa ajili ya kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji hivyo kwa kuwaunganishia umeme wa jua (Solar)”. Amesema, Mhandisi, Dominick. 

Mhandisi, Dominick Mnaa aliyataja majimbo hayo saba (7) kuwa ni kuwa ni Geita Mjini; Geita Vijijini; Busanda; Nyang’wale; Chato; Bukombe na Jimbo la Mbogwe.

 

Kwa upande wa Mwakilishi wa kampuni hiyo Tanzania, Bi. Carol Wang kutoka kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd; amesema kampuni yao imejipanga ili kukamilisha Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 105 vya mkoa wa Geita kwa haraka na ametumia fursa hiyo kumshukuru Mkuu wa mkoa kwa kuahidi kuwapa usaidizi wa aina yoyote wakati wa utekelezaji wa Mradi huo. 

Share:

Sunday, October 13, 2024

TAMWA YAZINDUA TUZO ZA WAANDISHI WA HABARI ZA MAENDELEO “SAMIA KALAMU AWARDS”

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wamezindua Tuzo ya SAMIA KALAMU AWARDS yenye kubeba kauli mbiu ya “UZALENDO NDIO UJANJA”.


Tuzo hizo zitatolewa kwa wanahabari watanzania kwa lengo la kuhamasisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari.


Aidha, utoaji wa Tuzo hizi umelenga kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira ya nchi.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben leo tarehe 13 Octoba 2024 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kubainisha kuwa Tuzo hizo zitahusisha maudhui yaliyochapishwa kupitia magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni, Tuzo maalumu kwa vyombo vya habari na maafisa habari wa Serikali.


Pia Dkt Rose Tuzo hizo zinahusisha habari zilizochapishwa kati ya Januari 01 hadi Oktoba 26, 2024 na kueleza kuwa Tuzo hizo zimepewa jina la SAMIA KALAMU AWARDS ili kutambua na kuenzi historia ya kuwa na Rais wa kwanza mwanamke nchini na zinatarajiwa kutolewa Novemba, 2024.


Ameeleza kuwa Kutokana na Maendeleo ya tekinolojia na utandawazi uandishi wa habari nchini umekua ukijikita kwenye kuburudisha, kuhabarisha huku uandishi wa makala za kuelimisha zikiwa kwa kiwango kidogo ambapo vyombo vyingi vya habari nchini vimekuwa vikitangaza maudhui ya nje yasiyokidhi mahitaji ya hadhira ya kitanzania.


Kwa muktadha huo, TAMWA kwa kushirikiana na TCRA tiliamua kutoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari, watangazaji, wahariri, mameneja, maafisa habari, wamiliki wa vyombo vya habari, wahadhiri na watengeneza maudhui ya mitandaoni wapatao 2,054 kote nchini, kwa kipindi cha miezi mitatu.


Tuzo hizo zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa, Tuzo kwa Vyombo vya Habari na, Tuzo za Kisekta ambapo amelezo ya kina yanapatikana kupitia tovuti ya https://samiaawards.tz


Dkt Rose amebainisha kuwa vigezo vitakavyotazamwa ni Makala ziwe zinahusu masuala ya maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi na fursa zinazopatikana kutoka kwenye miradi mbalimbali.


Makala hizo ziwe zimechapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza kwenye vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania. Aidha, mwandishi lazima awe Mtanzania na makala iwe imefanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina. Vyanzo vya habari visipungue vinne na makala hazipaswi kuwa zimeshawahi kushindanishwa kwenye tuzo nyingine. Kwa kuzingatia ulinzi wa haki miliki, kazi zote zitakazowasilishwa kwa ajili ya mashindano ni lazima ziwe za kipekee na zifuate masharti ya haki-miliki ya mwandishi na kituo kilichozitangaza.


Mchakato wa upigaji kura utahusisha wananchi kwa asilimia 60 na majaji kwa asilimia 40. Kura zitapigwa kupitia SMS SHORT CODE namba 15200 kupitia simu, na kutumia tovuti ingia link hii https://samiaawards.tz


Meneja wa huduma za utangazaji-TCRA Mhandisi Andrew Kisaka akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania-TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema kuwa lengo la tuzo hizo pia ni kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika makala zenye maudhui bora na zenye kuleta mabadiliko.


“Hizi ni tuzo za kipekee kwa sababu vyombo vya habari vyote vitashindishwa, maafisa habari nao watashindanishwa. Zitaleta matokeo chanya katika tasnia ya habari, Tunataka waandishi wa habari wanaoandika habari zenye kuleta mabadiliko “Quality local contents lengo ni kuongeza kiwango bora cha maudhui ya ndani", Amekaririwa Mhandisi Kisaka


MWISHO

Share:

Monday, September 23, 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo azungumzia Changamoto ya Rumbesa kwenye Zao la Vitunguu

 












WazoHuru Media - Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema kwamba Wizara itachunguza na kuondoa changamoto ya rumbesa katika zao la vitunguu ili kuwasaidia Wakulima kuepuka kuuza mazao yao bila kipimo cha uhakika. Kauli hiyo aliitoa Septemba 23, 2024, alipotembelea mashamba ya Wakulima wa vitunguu katika kata ya Ilkinding’a, Wilaya ya Arumeru, Mkoani Arusha.

Bw. Mweli alisisitiza kwamba Wakulima wa vitunguu wanaendelea kupambana kuhakikisha wanazalisha kwa wingi ili kusaidia taifa katika Usalama wa Chakula. Alisema ni jukumu la Wizara kuwahakikishia wakulima masoko yasiyo na changamoto, hivyo kuongeza uzalishaji na kipato chao.

“Nimekuja shambani kujifunza na kuona hali halisi. kunamambo yapo katika ngazi yangu na pia kwa viongozi wengine, nitaenda kushirikiana nao ili tuone namna ya kutatua changamoto hii ya rumbesa,” alisema Bw. Mweli.

Mwenyekiti wa Wakulima wa Vitunguu katika kata ya Ilkinding’a, Bw. Danieli Lukumai, alieleza kwamba wakulima wapatao 1,900 katika eneo hilo wanazalisha vitunguu katika ekari 1,980, huku wakizalisha tani 20,000 kwa mwaka, ambazo huuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, alisema changamoto kubwa ni kulazimika kuuza kwa mfumo wa rumbesa kutokana na kutokuwa na sheria za kuwabana wanunuzi.

Katika ziara hiyo, Bw. Mweli aliambatana na Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi,na Watendaji wengine wa Asasi hiyo kilele ya sekta binafsi inayojishughulisha na kuendeleza sekta ya horticulture nchini, ambaye alikaribisha ujio wa katibu mkuu, akisema kwamba ni mwanzo wa utatuzi wa changamoto za wakulima hao. Dkt. Mkindi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha hali ya wakulima.

Kuweka rumbesa ni kuzidisha ujazo wa mifuko ambayo ni mbinu inayotumiwa katika usafirishaji wa bidhaa, ambapo mfuko unakuzwa ili kuongeza ujazo wa bidhaa ndani yake. Hii inamaanisha kwamba, badala ya kutumia mifuko au kontena ya kawaida, wafanyabiashara au wakulima wanaweza kuamua kuongeza ujazo wa mifuko ili kuweza kubeba bidhaa nyingi zaidi ambapo Kuongeza ujazo kunaweza kusababisha bidhaa kuhifadhiwa vibaya, na hivyo kuathiri ubora wa mazao na Wakati mifuko inaongezwa ujazo, inaweza kuwa vigumu kudhibiti uzito halisi wa bidhaa, na hivyo kuathiri mauzo

Share:

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo afungua Maonesho ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani Mazao ya Kilimo - Arusha

                                 

Pichani: Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, akizungumza na wakulima na wadau mbalimbali waliojitokeza katika ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo, Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha)

                                 

                                     


Pichani:
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, akikagua teknolojia za uongezaji thamani ya mazao ya kilimo katika Maonesho ya Siku Mbili, akionesha dhamira ya serikali katika kuboresha uzalishaji na masoko kwa wakulima leo Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha)

                         

                           


Pichani: Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, akizungumza katika ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali leo Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha)



WazoHuru Media - ARUSHA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli,  Septemba 23, 2024 katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa (Mnara wa Mwenge - Arusha) amefungua Maonesho ya Siku Mbili ya Teknolojia za Uhifadhi na Uongezaji Thamani ya Mazao ya Kilimo baada ya mavuno, yaliyoandaliwa na Asasi Kilele ya Sekta Binafsi (TAHA) chini ya Mradi wa Feed the Future Tanzania yakilenga kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka

Katika hafla hiyo, Bw. Mweli alisisitiza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kumsaidia mkulima, akigusia jinsi Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha bajeti ya kilimo na kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima kupata teknolojia na masoko ya mazao yao.


Maonesho hayo yalijumuisha wadau mbalimbali kutoka katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka. Wakulima walipata fursa ya kujionea teknolojia za uvunaji, uhifadhi, usindikaji, uongezaji thamani wa mazao, na vifungashio vya kisasa, vyote vikilenga kuboresha ubora na kuongeza thamani ya mazao yao.


Wadau wa sekta hiyo walihamasishwa kuchangia mawazo na teknolojia zinazoweza kusaidia katika maendeleo ya kilimo endelevu, huku wakijadili mbinu bora za kuvutia masoko na kuongeza mapato yao. Maonesho haya yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini

Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, pamoja na serikali kwa kuendelea kusaidia upatikanaji wa teknolojia za uhifadhi na uongezaji thamani ya mazao ya kilimo. Dkt. Mkindi alisema ushirikiano huu ni muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini na kuboresha maisha ya wakulima.

Akiwa katika maonesho, Dkt. Mkindi aliahidi kwamba TAHA itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na serikali ili kuhakikisha malengo ya kuboresha uzalishaji na masoko yanafikiwa. Alisisitiza kwamba kwa pamoja, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo, hivyo kuwanufaisha wakulima na kuimarisha uchumi wa taifa

Share:

Tuesday, September 17, 2024

WAZIRI BASHUNGWA AMPA HEKO DKT BITEKO, ACHANGIA MIL 15 UBORESHAJI UWANJA WA KILIMAHEWA-BUKOMBE


Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amefunga mashindano ya mpira wa miguu ya KNK CUP 2024 yaliyotanguliwa na Bonanza la michezo mbalimbali ambapo amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko Kwa kuendelea kuunga mkono kwa kasi jitihada za Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya michezo nchini.


Waziri Bashungwa amesema Jitihada za Dkt.Biteko ambaye ni mbunge wa Jimbo la Bukombe zitasidia kukuza vipaji vingi Nchini hasa katika Wilaya ya Bukombe kwa kuwaweka pamoja vijana, kuimarisha afya na kuibua vipaji vyao.


Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye fainali hizo zilizofanyika katika uwanja wa Kilimahewa wilaya ya Ushirombo mkoani Geita tarehe 17 Septemba 2024 ameahidi kutoa kiasi Cha shilingi Milioni 15 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo.
 

"Nikupongeze kwa hatua hii ya kuendesha ligi Bora ndani ya WILAYA ya bukombe, hongera umeleta viongozi wakubwa wa michezo ambao wao wataweza kuchagua wachezaji wenye vipaji zaidi na kuwapeleka ligi kubwa za kitaifa" Amekaririwa Waziri Bashungwa


Kuhusu suala la miundombinu ya barabara, Bashungwa amemuhakikishia Naibu Waziri Mkuu huyo kuwa Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), tayari imeanza manunuzi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo – Katoro (km 59) kwa kiwango cha lami na kusisitiza hadi kufika mwishoni mwa mwezi Disemba 2024 kazi za ujenzi zitakuwa zimeanza.


Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt Doto Biteko amesema Uongozi wa Wilaya ya Bukombe umeandaa andiko la kutafuta wafadhili kwa ajili ya uboreshaji wa uwanja wa kilimahewa ikiwemo kuweka nyasi za kisasa.


"Na ninakushukuru Waziri Bashungwa Kwa kuanzisha huu mchakato wa uchangiaji kwa ajili ya uwanja huu na uwanja utajengwa kwa ubunifu mkubwa ili tupate kitu kizuri".Amesema Dkt. Biteko


Mashindano ya ligi ya KNK Cup 2024 yalishirikisha timu 246 kutoka Kata 17 za Wilaya ya Bukombe na kuandaliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa lengo la kuendeleza michezo katika Wilaya ya Bukombe na kuibua wachezaji wengi wenye vipaji na viwango.


Katika mashindano ya KNK Cup, 2024, Timu kutoka Kata ya Butinzya imebuka mshindi wa kwanza kwa ushindi wa goli 1 kwa 0 dhidi ya Timu kutoka Kata ya Bugerenga na kujinyakulua shilingi Milioni tano, jezi seti tatu, mipira mitatu na Kombe.


MWISHO
Share:
Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com