METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, September 17, 2024

WAZIRI BASHUNGWA AMPA HEKO DKT BITEKO, ACHANGIA MIL 15 UBORESHAJI UWANJA WA KILIMAHEWA-BUKOMBE


Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amefunga mashindano ya mpira wa miguu ya KNK CUP 2024 yaliyotanguliwa na Bonanza la michezo mbalimbali ambapo amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko Kwa kuendelea kuunga mkono kwa kasi jitihada za Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya michezo nchini.


Waziri Bashungwa amesema Jitihada za Dkt.Biteko ambaye ni mbunge wa Jimbo la Bukombe zitasidia kukuza vipaji vingi Nchini hasa katika Wilaya ya Bukombe kwa kuwaweka pamoja vijana, kuimarisha afya na kuibua vipaji vyao.


Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye fainali hizo zilizofanyika katika uwanja wa Kilimahewa wilaya ya Ushirombo mkoani Geita tarehe 17 Septemba 2024 ameahidi kutoa kiasi Cha shilingi Milioni 15 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo.
 

"Nikupongeze kwa hatua hii ya kuendesha ligi Bora ndani ya WILAYA ya bukombe, hongera umeleta viongozi wakubwa wa michezo ambao wao wataweza kuchagua wachezaji wenye vipaji zaidi na kuwapeleka ligi kubwa za kitaifa" Amekaririwa Waziri Bashungwa


Kuhusu suala la miundombinu ya barabara, Bashungwa amemuhakikishia Naibu Waziri Mkuu huyo kuwa Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), tayari imeanza manunuzi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo – Katoro (km 59) kwa kiwango cha lami na kusisitiza hadi kufika mwishoni mwa mwezi Disemba 2024 kazi za ujenzi zitakuwa zimeanza.


Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt Doto Biteko amesema Uongozi wa Wilaya ya Bukombe umeandaa andiko la kutafuta wafadhili kwa ajili ya uboreshaji wa uwanja wa kilimahewa ikiwemo kuweka nyasi za kisasa.


"Na ninakushukuru Waziri Bashungwa Kwa kuanzisha huu mchakato wa uchangiaji kwa ajili ya uwanja huu na uwanja utajengwa kwa ubunifu mkubwa ili tupate kitu kizuri".Amesema Dkt. Biteko


Mashindano ya ligi ya KNK Cup 2024 yalishirikisha timu 246 kutoka Kata 17 za Wilaya ya Bukombe na kuandaliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa lengo la kuendeleza michezo katika Wilaya ya Bukombe na kuibua wachezaji wengi wenye vipaji na viwango.


Katika mashindano ya KNK Cup, 2024, Timu kutoka Kata ya Butinzya imebuka mshindi wa kwanza kwa ushindi wa goli 1 kwa 0 dhidi ya Timu kutoka Kata ya Bugerenga na kujinyakulua shilingi Milioni tano, jezi seti tatu, mipira mitatu na Kombe.


MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com