METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 23, 2024

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo azungumzia Changamoto ya Rumbesa kwenye Zao la Vitunguu

 












WazoHuru Media - Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema kwamba Wizara itachunguza na kuondoa changamoto ya rumbesa katika zao la vitunguu ili kuwasaidia Wakulima kuepuka kuuza mazao yao bila kipimo cha uhakika. Kauli hiyo aliitoa Septemba 23, 2024, alipotembelea mashamba ya Wakulima wa vitunguu katika kata ya Ilkinding’a, Wilaya ya Arumeru, Mkoani Arusha.

Bw. Mweli alisisitiza kwamba Wakulima wa vitunguu wanaendelea kupambana kuhakikisha wanazalisha kwa wingi ili kusaidia taifa katika Usalama wa Chakula. Alisema ni jukumu la Wizara kuwahakikishia wakulima masoko yasiyo na changamoto, hivyo kuongeza uzalishaji na kipato chao.

“Nimekuja shambani kujifunza na kuona hali halisi. kunamambo yapo katika ngazi yangu na pia kwa viongozi wengine, nitaenda kushirikiana nao ili tuone namna ya kutatua changamoto hii ya rumbesa,” alisema Bw. Mweli.

Mwenyekiti wa Wakulima wa Vitunguu katika kata ya Ilkinding’a, Bw. Danieli Lukumai, alieleza kwamba wakulima wapatao 1,900 katika eneo hilo wanazalisha vitunguu katika ekari 1,980, huku wakizalisha tani 20,000 kwa mwaka, ambazo huuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, alisema changamoto kubwa ni kulazimika kuuza kwa mfumo wa rumbesa kutokana na kutokuwa na sheria za kuwabana wanunuzi.

Katika ziara hiyo, Bw. Mweli aliambatana na Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi,na Watendaji wengine wa Asasi hiyo kilele ya sekta binafsi inayojishughulisha na kuendeleza sekta ya horticulture nchini, ambaye alikaribisha ujio wa katibu mkuu, akisema kwamba ni mwanzo wa utatuzi wa changamoto za wakulima hao. Dkt. Mkindi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha hali ya wakulima.

Kuweka rumbesa ni kuzidisha ujazo wa mifuko ambayo ni mbinu inayotumiwa katika usafirishaji wa bidhaa, ambapo mfuko unakuzwa ili kuongeza ujazo wa bidhaa ndani yake. Hii inamaanisha kwamba, badala ya kutumia mifuko au kontena ya kawaida, wafanyabiashara au wakulima wanaweza kuamua kuongeza ujazo wa mifuko ili kuweza kubeba bidhaa nyingi zaidi ambapo Kuongeza ujazo kunaweza kusababisha bidhaa kuhifadhiwa vibaya, na hivyo kuathiri ubora wa mazao na Wakati mifuko inaongezwa ujazo, inaweza kuwa vigumu kudhibiti uzito halisi wa bidhaa, na hivyo kuathiri mauzo

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com