METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 29, 2024

DKT.GWAJIMA: UKATILI WA KIJINSIA NI CHANZO CHA MIGOGORO KATIKA FAMILIA


Na Saida Issa,Dodoma.

SERIKALI imesema kuwa ukatili dhidi ya Watoto na ukatili wa kijinsia katika familia umechangia kuongezeka kwa migogoro ya kifamilia hususan kati ya wenza au wanandoa jambo lenye athari kubwa katika malezi na ustawi wa watoto wa familia na jamii kwa ujumla. 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum,Dkt.Dorothy Gwajima wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Familia Mei 15 ,2024 katika Mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo amesema hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022. 

Dkt. Gwajima amesema kuwa utafiti huo unaeleza kuwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wengi wamekimbia familia zao kutokana na migogoro ya wenza au wanandoa ambapo Taarifa ya utafiti inaonesha asilimia 27 ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili huku asilimia 12 ya wanawake wa umri huo walifanyiwa ukatili wa kingono.

Amesema asilimia 13 ya wanawake waliowahi kuwa na mume au mtu mwenye mahusiano katika kipindi cha miezi 12 kabla ya utafiti huo walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono na kihisia.

Amesema kuwa unyanyasaji wa kimwili, kingono, au kihisia miongoni mwa wanawake walioolewa umepungua kutoka asilimia 50 mwaka 2015/16 hadi asilimia 39 mwaka 2022/23.

Hata hivyo Dkt.Gwajima amesema kuwa Wizara imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii lililopo Makao Makuu ya Wizara, Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Jumuiya. 

Amebanisha kuwa,Kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Jumla ya mashauri 14,600 yalishughulikiwa ambapo, yaliyohusu migogoro ya ndoa yalikuwa 5,306 (36%), yaliyohusu migogoro ya kifamilia na matunzo ya Watoto 5,944 (41%), yaliyohusu matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa yalikuwa 3,350 (23%).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com