METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 13, 2023

UTEKELEZAJI WA MIRADI WATAKIWA KUWEKWA WAZI


Ushirikiano na uwazi vimetakiwa kuzingatiwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopata fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.1 katika robo ya kwanza ili fedha zilizoletwa zitumike vizuri na kusaidia katika kutatua changamoto zingine.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kondoa Mhe. Mohamed Kiberenge wakati wa kikao cha baraza la Waheshimiwa madiwani robo ya kwanza kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Kondoa hivi karibuni.

“Waheshimiwa Madiwani tunapaswa kuwa karibu na miradi tusiwaachie wataalam peke yao twende tukasimamie ili miradi ikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa na si lazima fedha iliyoletwa iishe yote na hili linawezekana tukisimamia vizuri,”amesema Mhe. Kiberenge

Ameongeza kuwa mahitaji halisi yajulikane mapema ili kujua kiasi cha fedha kitakachotumika na ikibaki itasaidia kwenye kutatua changamoto zingine na kwa kutumia fedha kinyume ni kutowatendea haki wananchi wengine wenye mahitaji.

“Madiwani ndio wenyeviti wa maendeleo wa kata hatutegemei mradi ulioletewa fedha usikamilike na ambao hadi sasa kamati hazijaundwa mkaziunde ili TAKUKURU pia wanaopita huko wakatoe elimu kwa kamati hizo na penye changamoto msisite kuomba ushauri ili mambo yasikwame,”amesisitiza Mhe. Kiberenge

Akiongea Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi amewataka maafisa tarafa kwenda kushirikiana na watendaji wengine katika maeneo yao ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwani kwa kuongeza nguvu na kufanya kazi kwa pamoja usimamizi utakuwa mzuri na miradi itakamilika kwa wakati ikiwemo miradi yenye afya ambayo ndio imeonekana kuwa na changamoto zaidi.

“Tumefanya kazi ya usafi mitaani lengo lilikuwa kuwafanya wananchi waelewe dhana ya usafi sababu tumegundua wananchi wengi wanafanya usafi katika nyumba zao na si maeneo ya wazi au mifereji hawafanyi hivyo afisa mazingira hakikisha unasimamia usafi wa mji na chukua hatua za kisheria kwa wote wanaochafua mazingira na kufanya agenda ya afya kuwa ni ya kila siku ikiwemo kupanda miti na kuitunza,”amesema Dkt. Mkanachi

Akitoa taarifa ya mapokezi ya fedha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Ndg. Paul Sweya amesema Halmashauri imepokea shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, umaliziaji wa zahanati za Mulua na Choka na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya sehemu za kutolwa huduma za afya kwa kipindi cha robo ya kwanza.

“Naomba waheshimiwa madiwani mkatusaidie kuhamasisha wananchi wakachangie nguvu zao na ulinzi wa miundombinu hiyo pamoja na vifaa vya ujenzi sababu ni kwa manufaa yao lakini pia  kuendana na   kasi ya serikali na mapenzi ya serikali kwa wananchi wake,”amesema Mkurugenzi Sweya

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kondoa Ndg. Hija Sulu amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha zote hizo kwa kipindi cha robo ya kwanza na kuwataka watendaji kuacha tabia ya kufanya kazi kwa kwa mazoea zaidi ni kushirikishana palipo na changamoto ili zifanyiwe kazi.

Baraza la Waheshimiwa Madiwani robo ya kwanza limefanyika ambapo limehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya na kamati ya Usalama, viongozi wa taasis za serikali zilizopo Kondoa, Wakuu wa Idara, Wananchi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com