METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, November 20, 2023

NEC YAKUTANA NA WADAU WA UCHAGUZI MKOANI TABORA


Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewaasa wakazi wa maeneo yaliyoteuliwa kwa ajili ya majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo ambalo linalenga kupima utayari wa mifumo na vifaa vya uboreshaji wa Daftari.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika mkoani Tabora leo tarehe 20 Novemba, 2023 Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri amewapongeza wakazi wa mkoa huo kwa mkoa wao kuwa miongoni mwa mikoa miwili ambayo kata zake zimeteuliwa kufanya majaribio hayo ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.

Mhe. Mapuri amezitaja kata zitakazofanya majaribio hayo kuwa ni Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, ya mkoa wa Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, katika Mkoa wa Mara.

“Tume inawapongeza wakazi wa Mkoa wa Tabora kwa mkoa wenu kuteuliwa kuwa mwenyeji wa zoezi hili la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” amesema Mhe. Mapuri.

Ameongeza kwamba uboreshaji wa majaribio kwenye kata hizo utafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura ambapo vituo 10 vipo katika Kata ya Ng’ambo na vituo sita vipo katika Kata ya Ikoma.

Ameeleza kwamba vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Majaribio ya uboreshaji yatahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kundi lingine litakalohusika kwenye zoezi hili ni; wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com