METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, September 14, 2023

SILAA AHIMIZA WAKUU WA MIKOA KUTEKELEZA MAAMUZI YA BARAZA LA MAWAZIRI VIJIJI 975

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza na uongozi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara alipokwenda kufuatilia utekelezaji wa Maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 

 

 Sehemu ya viongozi na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya ya Nanyumbu mkoa wa Mtwara wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (hayupo pichani) alipokwenda kufuatilia utekelezaji Maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusina na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 13 Septemba 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na Munir Shemweta, WANMM NANYUMBU

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amehimiza wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha wanatekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975

‘’Niwaombe wakuu wa mikoa wote nchini kuendelea kusimamia utekelezaji maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya vijiji 975’’. Alisema

Waziri Silaa alisema hayo tarehe 13 Septemba 2023 wakati akizungumza na uongozi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara akiwa kwenye ziara ya siku moja kufuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya  matumzi  ya adhi katika vijiji 975.

Alisema, ameridhishwa sana na tekelezaji wa maamuzi hayo kwa mkoa wa Mtwara kupitia wilaya ya Nanyumbu ambapo kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi wilaya hiyo imeweze kutekeleza maagizo hayo kwa asiliamia mia moja.

Kwa mujibu wa Silaa, atahakikisha serikali inapotoa kauli lazima itekelezeke kwa kuwa ndiyo kazi aliyotumwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuweka bayana kuwa, kazi aliyotumwa ataifanya mapema na kupeleka majibu ya mpango wa serikali kwa wananchi wa Nanyumbu ili kupunguza taharuki.

‘’Mimi naamini utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri utakamilika kwa haraka kwa sababu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni maelekezo mahsusi ya Rais Samia kuwa, wizara ihakikishe jambo hili linafika mwisho’’ alisema Waziri Silaa

Aidha, alibainisha kuwa, migogoro ya ardhi inahusisha watu na pale utatuzi wake unapocheleweshwa unaleta mgogoro mwingine mkubwa kuliko wa awali jambo alilolieleza utatuzi wake unaweza kuwa mgumu kwa sababu utatuzi wa pili unaondoa imani ya wananchi kwa jambo lililoamuliwa na serikali kuwa linaweza kutekelezeka kwa haraka.

‘’Kwa kuwa kamati ilishaenda maeneo yote kasoro Peramiho, wajibu wangu ni kupita maeneo yote kwenda kuangalia utekelezaji maagizo ya Baraza la Mawaziri na nikiri tu utekelezaji wa maamuzi hayo kwa baadhi ya maeneo unasuasua’’ alisema.

Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 yanafuatia timu iliyoundwa kuchunguza changamoto za uvamizi wa maeneo ya hifadhi ambapo timu hiyo iliwasilisha taarifa ya migogoro katika vijiji 366 na ndipo ikaundwa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta mwaka 2019 iliyokuja na mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 huku vijiji 55 utatuzi wake ukisalia.

Wizara za kisekta zinazohusika katika utatuzi huo ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama mwenyekiti, Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Maji, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), TAMISEMI na Wizara ya Ulinzi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com