Imeelezwa kuwa Kiwanda cha Kusafisha dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) kinachomilikiwa na Mwekezaji Mtanzania Sarah Masasi kimeiweka Tanzania katika Soko la Kimataifa katika usafishaji wa dhahabu duniani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde Septemba 25, 2023 Mkoani Geita baada ya kutembelea na kuzungumza na mwekezaji na wafanyakazi wa kiwanda cha kisasa cha kusafisha madini ya dhahabu cha GGR.
Waziri Mavunde amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kiwanda hicho kupata Ithibati ( ISO Certification) za aina tano ikilinganishwa na kiwanda kikubwa cha kusafisha madini ambacho hakina ISO zote hizo.
Pia, Waziri Mavunde ameiagiza timu ya wataalam iliyoundwa ikihusisha wataalam kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Madini, wawakilishi wa wachimbaji wadogo na wamiliki wa viwanda vya usafishaji wa madini kuandaa taarifa itakayoelezea namna bora ya upatikanaji wa malighafi na ushiriki wa BoT kwenye kuwasaidia wachimbaji wadogo kuzalisha dhahabu itakayopelekwa kwenye viwanda hivyo.
" Dhahabu itakayosafishwa kwenye viwanda hivi sehemu ya uzalishaji huo itanunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania," amesema Mavunde.
Aidha, amesema kuwa ili kuwezesha kiwanda hicho kupata malighafi ya kutosha amemuagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Madini kuitisha kikao na wadau wote wanaomiliki leseni za madini ili kuzungumza kwa pamoja na hatimaye viwanda vya usafishaji madini ya dhahabu vya ndani ya nchini vipate malighafi ya kutosha.
Kwa upande wake, Mmiliki wa Kiwanda hicho cha Geita Gold Refinery (GGR) Mama Masasi ameishukuru Serikali kwa kumpatia ushirikiano katika kipindi chote kuanzia ujenzi hadi kukamilika na kuanza usafishaji wa dhahabu katika ubora wa 999.9.
"GGR tupo tayari kufanya kazi na Wachimbaji wote wa madini ili kusafisha dhahabu yao katika kiwanda hiki kwa kuwa kimekidhi vigezo muhimu vya kimataifa," amesema Mama Masasi
Naye, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Mheshimiwa Costantine Kanyasu amesema kuwa anatamani kumuona mwekezaji huyo anafanikiwa katika kiwanda hicho na kusisitiza Serikali iendelee kumpa ushirikiano katika shughuli zake.
Aidha, ameomba tafiti zifanyike zaidi ili wachimbaji wapate maeneo mengi ya kuchimba madini na hatimaye kiwanda hicho kiweze kupata mzigo kutoka kwa wachimbaji wa madini ili kuongezwa thamani.
Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula na watendaji wengine wa Wizara ya Madini na Taasisi zake.
0 comments:
Post a Comment