METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, July 2, 2023

WAZIRI MHAGAMA AKABIDHIWA KIPANDE CHA SEHEMU YA UJENZI WA UWANJA WA MASHUJAA


Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amekabidhiwa kipande cha sehemu ya ujenzi wa uwanja wa mashujaa, katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma mapema Julai 2, 2023.

Ujenzi huo unaotekelezwa na kampuni ya SUMA JKT,Umekamilisha kipande cha  sehemu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja wa Gwaride ambao unategemewa kutumika katika Maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Julai 25, 2023.

Akiwa kiwanjani hapo Waziri Mhagama alisema, Serikali pamoja na kuhamia Dodoma imejenga miundombinu yenye hadhi ya makao Mkuu ya Serikali, na jamii inashuhudia majengo ya Serikali makubwa na miondombinu mingine ikiendelea kukamilishwa.

Akiongelea Ujenzi wa Uwanja huo, Waziri Mhagama alisema, ujenzi utakapo kamilika utakuwa ni wa mfano Barani Afrika.

"Eneo hili ni sehemu ya kwanza ya ujenzi wa eneo la maadhimisho ya uwanja wa mashujaa, (Parade Ground) ambayo itakuwa na Mnara wa Mashujaa, wenye ubora na viwango vya juu kabisa.” Alieleza Mhe. Mhagama

Aliendelea kusema kuwa, awamu ya pili itakuwa na bustani kubwa, ambayo itakuwa na mvuto wa aina yake, na tayari Taasisi mbali mbali za Serikali zimeonesha nia ya kuwekeza na kushirikiana, kuhakikisha kutakuwa na bustani hiyo yenye migahawa, viwanja vya michezo na burudani mbalimbali, ambazo zitakuwa katika eneo hilo ambao leo amekabidhiwa kipande kidogo tuu kama sehemu ya kwanza ya ujenzi.

Alifafanua zaidi kuwa, sehemu ya tatu itahusisha ujenzi wa mnara mrefu wa zaidi mita 110 ambao utakuwa mnara wa kwanza Barani Afrika, ambao utakuwa ni kivutio kwa watalii na kuongeza pato la Taifa.

Kwa Upande Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi alisema uwanja huo utakapokamilika utaongeza uzuri na ubora wa Jiji la Dodoma na Serikali itahakikisha kwamba mnara pamoja na uwanja wake unakuwa wa kupendeza na kuwa na mvuto wa kipekee huku akizishuruku sekta nyingine zilizoonesha ushirikiano katika utekelezaji wa ujenzi huo na kuhakikisha miundombinu muhimu inapatikana kwa wakati.

Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma Bw. Meshach Bandawe, alisema ujenzi huo umezingatia suala la mpango kabambe wa ujenzi wa Mji wa Serikali na kazi ya ubunifu wa awali ilifanywa kwa kina na wataalam kutoka chuo kikuu cha Ardhi, TPA, NHC  na SUMA JKT.

Naye Mwakilishi wa kampuni ya Ujenzi kutoka SUMA JKT kanda ya Kati Meja Samweli Jambo, alisema ujenzi huo umefuata taratibu zote za upimaji na viwango.

 “Tulifanya kazi usiku na mchana kuhakikicha tunatekeleza maelekezo ya Mhe. Waziri ya kukabidhi kipande hiki kwa wakati.” Alieleza Samweli

  MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com