METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, May 18, 2023

VIJIJI VYOTE VILIVYOPO WILAYA YA KARATU NA MONDULI KUFIKIWA NA UMEME.



Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeendelea na hatua ya kusambaza umeme katika maeneo ya Wilayani Monduli na Karatu ili kuhakikisha Vijiji ambavyo havijafikiwa umeme vinafikiwa.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, aliyasema hayo, Mei 16, 2023  wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Mto wa Mbu (Monduli) na Karatu, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango inayoendelea Mkoani Arusha.

Aidha, Byabato amesema katika Wilaya ya Monduli Vijiji vitatu ambavyo havijafikiwa na  umeme, Mkandarasi anaendelea na kazi katika vijiji hivyo wakati Wilaya ya Karatu ni vijiji sita tu ambavyo pia  havijafikiwa na umeme, kazi ya kuvifikishia umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili inaendelea.

"Serikali kupitia Wakala wa Nishati  Vijijini (REA), itahakikisha vijiji hivyo vinapata umeme wa uhakika ili wananchi waweze kufikiwa na huduma hiyo"amesema Byabato.

Hata hivyo, amesema kuwa  Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 109 kwaajili ya kuendelea kusambaza umeme katika Mkoa wa Arusha, katika maeneo ya Mjini na Vijijini, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo uzalishaji kwenye maeneo ya Migodi, Mashamba ya Umwagiliaji na pampu za Maji.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com