METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 1, 2023

WAZIRI BASHUNGWA ATETA NA WAZEE WA JAMII YA KIMASAI WATUMA SALAMU ZA PONGEZI KWA RAIS DKT. SAMIA

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutunza na kuenzi mila na desturi za Kitanzania ambazo zinaimarisha amani na upendo kwa Watanzania.

Bashungwa ameyasema hayo tarehe 01 Machi 2023 katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha katika Kikao na Wazee wa Jamii ya kimasai kilicholenga kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo na Kudumisha amani nchini.

Bashungwa ametoa wito kwa Wazee wa Jamii ya Kimasai kuendelea kusimamia na kuikumbusha jamii hasa Vijana kudumisha mila na desturi za kitanzania ambazo ni utambulisho wa Taifa la Tanzania.

Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi za maendeleo katika wilaya Monduli na maeneo yote nchini huku akisisitiza kuwa miradi inaendelea kutekelezwa ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Kwa upande wao, Wazee wa Jamii ya Kimasai katika eneo la Monduli wamemshukuru Mheshimiwa  Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoendelea kuifanya kwa kutoa fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya ya Monduli.

Kwa kauli moja wazee hao wameunguna na kutuma Salamu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huku wakisisitiza kuwa aendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuifanya Tanzania kuzidi kuimarika katika maendeleo.

Kadhalika, Wazee hao wamesema wanataka kuona ifikapo mwaka 2025  jina la mgombea Urais liwe moja tu la Dkt. Samia ili waweze Kulipa fadhila kwa kazi anazozifanya kwa manufaa ya watanzania wote.

Mwisho
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com