METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 2, 2022

JKT KUJA NA MKAKATI WA KUTENGENEZA AJIRA KWA WAHITIMU WA MAFUNZO: BASHUNGWA

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) amesema Jeshi la Kujenga Taifa litapanua wigo wa Kazi kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta kuweka Mkakati wa pamoja kutengeneza ajira kwa Vijana wanaomaliza Mafunzo ya kujitolea katika Jeshi la kujenga Taifa.

Ameyasema hiyo Bungeni Jijini Dodoma tarehe 02 Novemba 2022 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Malinyi, Mhe Antipas Mgugusi aliyetaka kujua ni agizo gani la Serikali la kutoa Kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa mafunzo JKT.

“Jeshi la Kujenga Taifa tunataka tupanue Mawanda (scope) kwa kushirikisha sekta nyingine kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Wizara ya Mifugo na taasisi nyingine kuweka mkakati wa kusaidia kutengeneza ajira kwa vijana wanaomaliza mafunzo ya kujitolea na kurudi mtaani” amesema Bashungwa

Bashungwa amesema ameunda Kamati Maalum katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo itashirikiana na Wizara nyingine za kisekta na taasisi zake na kuja na mkakati wa pamoja wa kuongeza wigo wa ajira za vijana wanaojitolea.

Awali wakati akijibu Swali la Msingi, Bashungwa amesema mnamo mwaka 2013, Serikali ilitoa maelekezo kwa Wizara zote pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ambapo utaratibu huo umekuwa ukitekelezwa.

Bashungwa ameeleza kuwa lengo la mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwapatia vijana wa Tanzania elimu ya Uzalendo, Ujasiliamali na kujifunza stadi za kazi ili waweze kijiajiri mara wanapomaliza mkataba.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com