METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 12, 2022

WAZIRI MKENDA AZINDUA TUZO YA TAIFA YA MWALIMU NYERERE YA UANDISHI BUNIFU//MIL 22 KUTOLEWA KWA WASHINDI WATATU WA JUU


Na Mathias Canal, WEST-Dar es salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amezindua Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi bunifu iliyofanyika katika ukimbi wa mikutano wa Benki ya CRDB Jijini Dar es salaam leo tarehe 12 Septemba 2022.

Tuzo hiyo itatolewa kwa kazi mahiri yenye Sanaa ya kina itakayoshinda katika shindano hilo na mshindi wa kwanza atapokea kitita cha Shilingi Milioni 10, Mshindi wa pili Shilingi Milioni saba, na Mshindi wa tatu atapokea shilingi Milioni 5.

Akizungumza na wadau waliohudhuria katika hafla hiyo Waziri Mkenda amesema kuwa Tuzo hiyo itatolewa Aprili 13 mwakani baada ya uchambuzi wa kina wa kazi zote za Sanaa zitakazowasilishwa na waandishi.

“Tuzo ni lazima iende kwa mwandishi mwenye Sanaa ya kina sio kulipua kwa kuandika masaa mawili au matatu au manne au mwezi, ziwe ni kazi zenye kutumia akili nyingi na sio mapambio wala mabezo” Amesisitiza Waziri Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa waandishi wanapaswa kuhakikisha kuwa kazi hizo zinakuwa ni zile zinazokuza utamaduni na fahari ya nchi na ubora wa hali ya juu.

“Kuna watu wakisikia majaji na wakiwajua tu wanaanza kupiga simu ili wapewe ushidni, sasa mara mia tuzo isitolewe na kuacha mwaka huu upite wakati tunajipanga lakini tusitoe kwa upendeleo wowote, Lakini kwa kuwa mmenihakikishia kuwa tayari watu wameanza kuandika basi vyema haki itendeke” Amekaririwa Waziri Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa Tuzo hiyo imepewa jina la Muasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya waandishi bunifu ikiwa ni sehemu ya kuenzi weledi wake na ufanisi wa lugha ya Kiswahili katika uandishi aliokuwa akiufanya.

Tunatumia jina la Mwalimu Nyerere ili kuendeleza haki miliki ya jina hili, tunatumia kwa kuwa ni msomi na mwandishi mzuri wa mashairi na tungo mbalimbali.

Waziri Mkenda amesema kuwa kupitia tuzo hiyo itakayokuwa inatolewa kila mwaka itajikita na kuhakikisha kuwa inakuza utamaduni wa Taifa na Lugha ya Kiswahili.

Pamoja na kuwapongeza wajumbe wote walioshiriki katika uandaaji wa tuzo pia amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt Aneth Komba kwa kusimamia kwa ufanisi mkubwa utekelezaji na uwezeshaji wa maandalizi ya tuzo hiyo.

 

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com