METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, August 11, 2022

ZIMAMOTO YAFANYA MABADILIKO TOZO ZA UKAGUZI WA USALAMA DHIDI YA MAJANGA

 

KAMISHNA Msaidizi Mwandamizi  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ,Puyo Nzalayaimisi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu mabadiliko ya tozo za ukaguzi wa usalma  dhidi ya majanga ya moto leo Agosti 11,2022 jijini Dodoma 

JESHI la Zimamoto na Uokoaji,limebadilisha tozo za ukaguzi wa usalama dhidi ya majanga ya moto katika Majengo na maeneo mbalimbali pamoja na utaratibu wa ukusanyaji wa tozo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 11,2022 jijini Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ,Puyo Nzalayaimisi amesema kuwa kuanzia mwezi julai tozo zimebadilika Sanjari na mabadiliko ya utaratibu wa ukaguzi.

“Hivyo wananchi watambue kuna mabadiliko ya gharama za tozo katika maeneo mengi mfano maduka, viwanda, makazi, ofisi, shule, nyumba za kuishi, usomaji wa ramani pamoja na gharama za usajili wa makampuni yanayojishughulisha na utoaji huduma za kuuza vifaa, uwekaji wa vifaa vya kuzima moto pamoja na mifumo ya uzimaji moto,”amesema.

Pia Nzalayaimisi alisema kuwa pamoja na kushuka kwa gharama za tozo kuna maingizo mapya ya tozo ikiwa ni sehemu za karakana, vituo vya usafirishaji na wanaofanya biashara ya kufua nguo (dry cleaner ).

“Hata hivyo zipo baadhi ya tozo ambazo zimefutwa mfano transformer, mashamba ya kahawa, mkonge pamoja na chai, haya ndio mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika juhudi za kuinua sekta ya kilimo,”amesema

Aidha ameongeza kuwa Tozo hizo zinakusanywa kwa mujibu Sheria namba 14 ya mwaka 2007 “The Fire and Rescue Force Act”, ikisomwa pamoja na Kanuni ya ukaguzi na vyeti ya mwaka 2008 pamoja na mabadiliko ya mwaka 2022 iliyoainisha mabadiliko hayo.

Amefafanua kuwa awali Jeshi hilo lilibeba jukumu la kumfuata mteja na kuomba kufanya ukaguzi katika Jengo, eneo au chombo cha usafiri lakini kwa sasa Utaratibu huo umeboreshwa zaidi ili kuleta tija na kuliwezesha Jeshi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

“Kanuni tajwa ya ukaguzi na vyeti imeelekeza kuwa ni wajibu wa mteja/mmiliki wa jengo, eneo au chombo cha usafiri ambaye hajafanyiwa ukaguzi kufika ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuomba kukaguliwa,”amesema.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com