Na Maganga Gwensaga – Dodoma
Mwenyekiti wa kamati ya Sensa ya Wilaya ya Kongwa na
Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Remidius Mwema amewataka makarani, wasimamizi wa
maudhui na Tehama Kila mmoja kutambua
thamani ya uwepo wake katika mafunzo hayo, ajifunze kwa makini ili
kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Mwenyekiti huyo alisema hayo Julai 31, 2022 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya makarani,
wasimamizi wa Tehama na maudhui ambao watashiriki katika zoezi la sensa ya watu
na makazi litakalofanyika nchini tarehe 23 Agosti mwaka huu.
“ Ndugu zangu naomba niwaeleze, wewe uliyeko hapa
utambue thamani kubwa uliyopewa na Serikali ya kushiriki zoezi hili kubwa la
Kitaifa ambalo linaenda kufanyika nchini kwetu na hauko hapa kwa bahati mbaya.”
Alisema Mwema
Alisema zoezi la Sensa ni muhimu sana kwani ni
maendeleo, ni elimu, ni barabara, ni
afya , ni umeme hivyo kuzingatia kwao mafunzo kutasaidia ukusanywaji wa taarifa
sahihi za watu na makazi hivyo watairahisishia Serikali katika masuala ya kupanga
mipango yake ya kimaendeleo ambayo imekusudia kuwapelekea wananchi wake.
“ Serikali inawategemea sana, usipozingatia mafunzo
ukafanya mzaha katika jambo hili na mwisho wa siku ukafanya ndivyo sivyo, zoezi
letu likaharibika wewe ndio utakuwa sababu kumbuka sio Kongwa tu, wala Dodoma bali
utakua umeharibu taswira nzima ya zoezi hili Kitaifa na nisingependa yatokee
hayo.” Aliongeza.
Aidha
aliwataka washiriki hao kuzingatia muda uliowekwa wa kuanza mafunzo ili
muda uliotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu uende sambamba na muda wa mafunzo
ili yaweze kukamilika kwa wakati, uku akisisitiza kufanya kazi kwa weledi, kuwa
na nidhamu pamoja na kuheshimiana.
“ Suala la nidhamu ni muhimu sana najua wengine
mnatofautiana umri, vyeo nk hivyo ni vyema kuheshimiana, kuzingatia muda wa
kuja, kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe, kutii walimu wenu, kusikiliza kwa
umakini na kujiepusha na vitendo vyote ambavyo viko kinyume na maadili.”
Alisema
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo
wamemuhakikishia Mwenyekiti huyo kuzingatia mafunzo yote watakayopewa na
wakufunzi hao na wako tayari kushiriki na kufanikisha zoezi hilo.
Mafunzo ya makarani, wasimamizi wa maudhui na Tehama
yalianza Julai 31 Agosti na yanatarajia kumalizika tarehe 18 Agosti nchi nzima ambapo
kwa Wilaya ya Kongwa yamegawanywa katika vituo vinne(4) ambavyo ni Kongwa,
Kibaigwa, Mlali na Mkoka ambapo yatatolewa kwa makarani 1197, Wasimamizi wa
Tehama 22 na Wasimamizi wa Maudhui 24.
Ikumbukwe wilaya ya Kongwa ndio wilaya pekee ambayo
itakuwa na matukio makubwa mawili siku hiyo, mosi uwepo wa zoezi la Sensa ya
watu na Makazi pamoja na pili ni Mbio za Mwenge wa uhuru.
0 comments:
Post a Comment