Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wakaguzi wa ndani Sekta ya Maji.
Mwenyekiti wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Maji Tanzania, CPA. Beatus Gulabaganira akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa kikao kazi cha wakaguzi wa ndani Sekta ya Maji.
Baadhi ya wakaguzi wa ndani kutoka taasisi mbalimbali katika Sekta ya Maji wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (aliyesimama) akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wakaguzi wa ndani Sekta ya Maji. Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Maji, CPA Paul Temba akizungumza kabla ya ufunguzi wa kikao kazi cha wakaguzi wa ndani Sekta ya Maji.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na sekretarieti ya kikao kazi cha wakaguzi wa ndani Sekta ya Maji.
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wakuu wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji kuhakikisha Wakaguzi wa Ndani wanapata rasimali zote muhimu zitakazowawezesha kutekeleza wajibu wao kwa uhuru na ufanisi.
Waziri Aweso ametoa maelekezo hayo Juni 13, 2022 Jijini Mwanza alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku sita cha Wakaguzi wa Ndani wa taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Wakaguzi wa Ndani wa Sekta ya Maji Tanzania, CPA. Beatus Gulabaganira alibainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wakaguzi wa ndani wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuzipatia ufumbuzi.
CPA. Beatus alieleza kuwa Wakaguzi wa Ndani wa Mamlaka nyingi za Maji wamewekwa katika nafasi ya chini kimuundo ikilinganishwa na wakuu wa idara jambo ambalo linasababisha wasiwe huru pindi wanapokuwa na wajibu wa kumkagua Mkuu wa idara ambaye yupo juu kimamlaka.
Changamoto nyingine zilizowasilishwa na wakaguzi wa ndani katika kikao hicho mbele ya Waziri Aweso ni kutokuwa na vitendea kazi muhimu ikiwemo usafiri, kutokuwa na uelewa wa matumizi ya mifumo ya kielektroniki pamoja na miongozo mbalimbali kutokana na kutopewa mafunzo na kutopata fursa ya kushiriki vikao vikuu vya maamuzi vya taasisi suala ambalo linawasababishia kushindwa kutoa ushauri kabla maamuzi hayajafanyika.
Waziri Aweso alizipokea changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi ambapo aliwaelekeza wakuu wote wa taasisi za maji kutengeneza mazingira rafiki yatakayowezesha ofisi za wakaguzi wa ndani kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuleta tija iliyokusudiwa.
Akizungumzia suala la usimamizi wa miradi ya maji, Waziri Aweso aliwaelekeza wakaguzi wa ndani wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kama ilivyokusudiwa ili kuleta matokeo chanya.
Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha imani kubwa kwa Wizara ya Maji na kwamba ni jukumu la kila mtumishi katika Sekta ya Maji wakiwemo wakaguzi wa ndani kuhakikisha imani hiyo ya Mhe. Rais haipotei.
“Mmeshuhudia namna ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, alivyotuamini kwa kutupatia fedha nyingi za ujenzi wa miradi, ni wajibu wetu kuhakikisha hatuipotezi imani hiyo kwake kwa kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa weledi kwa kusimamia vyema ujenzi wa miradi,” alielekeza Waziri Aweso.
Aliwaelekeza kutumia ujuzi na uzoefu wao kujiuliza na kufuatilia endapo fedha iliyotengwa kwa dhumuni la kutekeleza miradi imetumika ilivyokusudiwa na kama inaleta matokeo chanya.
Waziri Aweso alisema kuwa wakaguzi wa ndani ni jicho la Wizara kwani kupitia wao hatua mbalimbali za utekelezwaji wa miradi na matumizi ya fedha kwenye ujenzi wa miradi unakuwa bayana na hivyo aliwataka kutambua jukumu lao la msingi bila kumuonea mtu.
“Mkaguzi wa ndani ni jicho la taasisi, sasa hakikisheni jicho hilo sio chongo; mnapaswa kumulika viashiria vyoyote vya matumizi mabaya ya fedha za miradi na kuishauri taasisi nini kifanyike sio kusubiri hadi mambo yaharibike,” alisisitiza Waziri Aweso.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini, aliwaasa wakaguzi wa ndani kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa weledi.
“Kwa niaba ya wenzangu tunaahidi kuendelea kushirikiana nanyi, kama alivyosema Mhe. Waziri Aweso ninyi ndio jicho letu msituangushe nasi hatutawaangusha tunatambua umuhimu wenu,” alisema Mhandisi Msenyele.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Maji, CPA Paul Temba alimshukuru Waziri Aweso kwa kutenga muda wake kuja kuzungumza na wakaguzi wa Ndani wa taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji licha ya kuwa na majukumu mengine mengi ya kitaifa.
0 comments:
Post a Comment