Na
Mathias Canal, WEST-Dodoma
Katika mageuzi makubwa ya
elimu yanayofanywa nchini serikali imekusudia kuzingatia kwa kiasi kikubwa
kuwajengea ujuzi wa kutosha wahitimu ili kuwarahisishia kuweza kuingia katika
soko la ajira ili waweze kuajiriwa au kujiajiri pasina kupoteza ubora wa elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amyeyasema hayo wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe Didie Chassot ofisini kwake
Jijini Dodoma Leo tarehe 1 Juni 2022.
Amesema kuwa ushirikiano
mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili hususani katika maeneo ya kuongeza ujuzi
kwa vijana na kuimarisha upatikanaji wa ajira pamoja na vyuo vya ufundi
utaendelea ili kuhakikisha kuwa nchi hizo mbili zinaimarika na kuwa na weledi
mkubwa katika sekta ya elimu.
Waziri Mkenda amesema kuwa endapo
baadhi ya mapendekezo yatachukuliwa kwenye mijadala mbalimbali inayoendelea nchini
ni pamoja na kuongeza nguvu na kuwekeza katika elimu ya ufundi na vyuo vya
ujuzi wa aina mbalimbali.
Amesema kuwa miongoni mwa
sekta ambayo Usiswi imejipambanua vizuri ni vyuo vya ukarimu na utalii hivyo
serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia
kuboresha zaidi mahusiano ya vyuo hivyo katika nchi zote mbili.
Amesisitiza kuwa serikali
inaangalia uwezekano mahususi wa kupeleka wakufunzi nchini Uswisi katika
kipindi kisichopungua mwezi mmoja ili kujifunza katika vyuo hivyo.
“Na nimewaalika kuleta
wakufunzi wao hapa nchini ili kukaa kwenye vyuo vyetu waweze kutueleza
wanachoona kama tunatoa huduma kwa ubora ule ambao unatakiwa”
Kadhalika, Waziri Mkenda
amewaalika wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali ambao wanaweza kuanzisha
vyuo hapa nchini hususani vya utalii kwani milango ya uwekezaji ipo wazi.
Kwa upande wake Balozi wa
Uswisi nchini Tanzania Mhe Didie Chassot amemuhakikishia Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda kuwa Uswisi itaendeleza ushirikiano
katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kuimarisha ujuzi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment