Na Mathias Canal, Dar es
salaam
Serikali imejipanga
kuhakikisha kuwa watoto wenye mahitaji maalum wanapata huduma zote stahiki
ikiwemo elimu kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.
Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 7 Machi 2022
mbele ya mgeni rasmi-ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Samia Suluhu Hassan wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye shule ya sekondari
Benjamini Mkapa Jijini Dar es salaam.
Prof Mkenda ametoa mwito
kwa watanzania wote hususani wazazi kutowawaficha ndani watoto wenye mahitaji
maalumu badala yake wawapeleke shule ili waweze kupata elimu.
"Katika uongozi wa
Rais wetu Mhe Samia Juhudi mbalimbali zinafanyika ili kuendeleza fursa kwa
wanafunzi kupata elimu bila kikwazo" Amekaririwa Prof Mkenda
Amesisitiza kuwa kwa
sasa serikali imekamilisha ujenzi wa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu
katika Wilaya ya Masasi mkoani Lindi pamoja na Arusha na shule nyingine ambayo
ujenzi wake unaendelea mkoani Geita.
Kadhalika, Waziri Mkenda
amesema kuwa ndani ya mwaka mmoja serikali imejenga vituo shikizi 3000 vya
kusomesha watoto ambapo kwa wale wasioweza kuifikia huduma ya elimu wanaweza
kufikishiwa popote walipo.
Amesema kuwa tayari
kamishna wa elimu Tanzania ametoa muongozo wa namna ya kuwapokea wanafunzi
ambao waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali ili warejee kusoma.
Waziri Mkenda
amemuhakikishia Rais Samia kuwa, tayari wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
imeanza kutekeleza maagizo aliyoyatoa kuhusu kupitia upya mitaala ya elimu kwa
ajili ya kuongeza ubora wa elimu na pia kuifanya elimu iweze kuakisi mahitaji
halisi ya nchi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment