METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 23, 2022

­­­WANAWAKE NA WASICHANA IKUNGI WAANZA KUNUFAIKA NA USAWA WA JINSIA

Afisa Jinsia kutoka Shirika la Farm Africa Hellena Lawi akitoa mafunzo kwa wanawake wa kata ya Sepuka Kuhusu haki za Mwanamke katika jamii kwenye maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani.


Diwani vitimaalum wa kata ya Sepuka  wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Halima Ng'imba akizungumza na waandishi wa habari. 


Katibu wa Madiwani Wilaya ya ikungi mkoani singida Hellena Ayoub akizungumza na baadhi ya wanawake walishiriki maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarafa ya sepuka.


Afisa Jinsia kutoka shirika la Farm Afrika akizungumza na waandishi wa habari  baada ya maadhimisho hayo.


Afisa Jinsia kutoka shirika la Farm Afrika akionesha cheti cha pongezi kutoka kwa wanawake wa kata ya Sepuka Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  wakati Maadhimisho ya siku ya wanawake dunia  kitarafa

HALMASHAURI  ya wilaya ya Ikungi mkoani Singida, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Farm Africa, kwa ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa la UN Women, imeanza kufanikiwa katika upatikanaji wa  haki wanawake  kumiliki ardhi  na kushiriki katika vikao vya maamuzi  zimeanza kuzaa matunda

Akizungumza kwenye Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniania iliyofanyika tarafa ya Sepuka, wilaya ya Ikungi mkoani Singida, ofisa jinsia wa Farm Africa, anayehusika na kumwezesha mwanamke kupitia mradi wa alizeti, Helena Lawi, alisema mradi huo umefungua fursa mpya kwa wanawake wa Ikungi juu ya upatikanaji wa haki zao.

“Huwezi kuwalinganisha wanawake na kipindi cha nyuma, kupitia mradi wa alizeti. Pia tunapongeza jitihada za Halmashauri ya Ikungi kufanikisha upimaji wa ardhi na wanawake sasa wanamiliki ardhi na wanadhibiti matumizi holela ya rasilimali, wanaingia kwenye vikao vya maamuzi…haya ni mageuzi makubwa ya maendeleo katika wilaya hii” alisema Bi Hellen

Bi Hellen Alisema mradi huo ulioanza miaka miwili iliyopita, hivi sasa umefanikiwa, ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, hali inayotoa dalili nzuri kwa kundi hilo kuweza kuinuka kiuchumi, sawa sawa na jinsia ya kiume.

 Aliongeza kubainisha kuwa Farm Africa mwaka huu imewezesha wakulima 427 (52% wanawake) kupata mbegu bora Kiasi cha Zaidi ya tani 4 ambazo zitawezesha wakulima wadogo kulima zaidi ya ekari 2000 katika katika vijiji vinne vya mradi vya Irisya, Munyu, Mnang’ana na Kimbumbuiko.

Diwani kata ya Sepuka Halima Ng’imba alisema kuwa, licha ya mafanikio hayo, wanawake wanapaswa kuongeza bidii ili kufikia lengo katika kuzingatia usawa wa kijinsia, hali itakayoimarisha uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Diwani Ng’imba alisema, pamoja na jamii ya nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania kuathiriwa na mila ama tamaduni zilizopitwa na wakati kutokana na baadhi kuwa na madhara kwa kundi hilo, wanawake na wasichana wanapaswa kujiongeza ili kuleta tija wilayani humo.

Hata hivyo alisema katika kukabiliana na changamoto hiyo, shirika la Farm Africa limeamua kujitosa kwa dhati kuliwezesha kundi hilo kiuchumi, kupitia njia ya kilimo, hivyo akawaomba wanawake kuliunga mkono katika vita hiyo.

Mgeni rasmi kwenye sherehe hizo zilizoandaliwa na mungano wa vikundi vya wanawake tarafa ya Sepuka, katibu wa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Helena Ayubu, alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Alisema, wanawake ni muhimili katika familia, kutokana na  nafasi mbalimbali zinazoongozwa na mwanamke kuwa na tija, akitolea mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan, alivyoweza kumaliza tatizo la vyumba vya madarasa kwa muda mfupi.

Vikundi mbalimbali vya wanawake, ikiwemo Wajifya, Mfuu, Mrumba na Masenga, vinajihusisha na mradi wa alizeti wilayani Ikungi, hivyo kufungua fursa mpya za kiuchumi na kupata soko la uhakika kwa zao hilo, hivyo kunufaisha mamia ya wanawake na familia zao.

Kwa mujibu wa afisa ushirika halmashauri ya wilaya ya Ikungi Gurisha Msemo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imegawa tani 95,132 kwa wakulima, kwa ajili ya kilimo cha alizeti msimu huu, ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini.

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com