METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 31, 2021

DC MWENDA ATATUA MGOGORO WA ARDHI WA ZAIDI YA MIAKA 10 WA HEKARI 420 ZA USHIRIKA NA KUZIGAWA NUSU KWA NUSU.




 Iramba, Singida.

Mkuu wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida Mhe. Suleiman Mwenda amesikiliza na kutatua mgogoro wa ardhi hekari 420 kati ya Wananchi na Chama cha Ushirika ambapo kila kundi lilidai kuwa hekari hizo ni zao. Mhe. Mwenda ametatua mgogoro huo leo Ijumaa Desemba 24, 2021 wakati alipokutana na viongozi wa Chama cha Ushirika na Wananchi wa kijiji cha Nkyala, Kizonzo na Nselembwe tarafa ya Shelui Wilayani hapa.

Tangu mwaka 1995 Chama cha Ushirika kiliyaacha mashamba haya mpaka leo hii ni takribani miaka 26 ambapo baadhi ya Wananchi waliyavamia na kuanza kuyatumia.

Akitolea ufafanuzi  baadhi ya sheria za ardhi, alisema kuwa mtu anapotumia ardhi kwa miaka 10 na zaidi na hapakuwa na yoyote wakumbuguzi au kumyang'anya basi eneo hilo linakuwa lakwake.

Katika kuhakikisha mgogoro huo unatatuka Mkuu huyo wa Wilaya alitoa maamuzi ya kuzigawa hizo hekari za ardhi.

"Ndugu zangu hekari 420 ni nyingi sana hivyo ninazigawa kuwa hekari 210 zitarudi katika Chama cha Ushirika na hekari 210 zibaki kwa Wananchi hawa.” Alisema Mwenda na kuongeza kuwa 

“Nawaomba muwe na imani kuwa haki yenu haitapotea kila mmoja atapata eneo ili muendelee na maisha ya kila siku, hivyo hekari hizi tutazigawa kwa utaratibu mzuri.”

Aidha, aliwataka Watendaji wa Vijiji kutokuwa chanzo cha kuibua migogoro ya ardhi kati yao na Wananchi hasa kwa kuuza ardhi ambayo haimilikiwi na Serikali ya kijiji.

“Kimsingi yapo makosa yaliofanyika kwa upande wa Chama cha Ushirika kwa kutoacha utaratibu mzuri wa kuyalinda mashamba yao,halikadhalika kwa upande wa Wananchi ambao wamengia kienyeji kwenye mashamba ya Ushirika.”

Pia aliwataka Wananchi hao kuhakikisha maeneo au mashamba yao yanapimwa kwa lengo lakuhakikisha mipaka inatambulika nakutosababisha migogoro.

“Ndugu zangu ni lazima sasa muhakikishe mashamba au nyumba zenu zinapimwa, eneo,  ardhi, bustani au nyumba inapokuwa imekwishapimwa inaongezeka thamani.” alisema.

Kutokuwa na hati miliki zinazotambulika kisheria baada ya miaka kadhaa ni kiashiria cha kuingia katika migogoro tena na Chama cha Ushirika na kama sio Chama cha Ushirika basi itakuwa wao kwa wao au na watoto wao kwa sababu watu wanazaliwa lakini ardhi haiongezeki.

Akiongea mbele ya mkuu huyo wa wilaya, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Singida, Angela Maganga alisema kuwa kwa sababu Wananchi hao wanaweza kuwa washirika katika Chama cha Ushirika basi wakubaliane na maamuzi hayo yatakayotolewa.

“Enyi ndugu zangu tambueni kuwa sisi tunawatazama kwa jicho la pili ambapo nyinyi ni wanufaika wa Chama cha Ushirika, tutakuja tuwape elimu ili mjisajili katika Ushirika na kuendelea kunufaika na mambo yanayopatikana katika Ushirika.” Alisema Maganga

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika (SIFAKU) Mkoani humo, Yahaya Hamisi alisema kuwa wanahitaji kuliendeleza shamba lao kwa kulima zao la alizeti ambayo ipo katika mpango wa kimkoa.

“Ni vyema mkatambua ndugu zangu  msimu huu tumepata mkopo toka benki ya TIDB kwa ajili ya kulima hekari 200.”

Naye mkazi na mdai wa eneo hilo, Rashidi Mayingule Alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa namna ambavyo ametatua mgogoro huo.

“Kwa kweli tunashukuru sana, leo tumepata ufumbuzi wa mashamba haya, hivyo tutaendelea na shughuli zetu za kilimo kwa sababu tayari mvua zimeanza.” Alisema


MWISHO.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com