METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, November 4, 2021

WAZIRI MKENDA AFUNGUA MKUTANO JIJINI DAR ES SALAAM KUHUSU MAJADILIANO YA KISERA KWENYE MAZAO YA MBEGU ZA MAFUTA

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, leo tarehe 4 Novemba 2021 Jijini Dar es salaam. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Bi. Amina Shaaban Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano wa majadiliano ya kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, leo tarehe 4 Novemba 2021 Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda na Bi. Amina Shaaban Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa majadiliano ya kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, leo tarehe 4 Novemba 2021 Jijini Dar es salaam.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akisalimiana na  Mkuu wa Kitengo cha Miradi inayafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) Wizara ya Fedha na Mipango mara baada ya kufungua mkutano wa majadiliano ya kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania leo tarehe 4 Novemba 2021 Jijini Dar es salaam.


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam


Serikali itaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta. Kwa upande wa alizeti imeanza kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kujitosheleza kwa mafuta ya kula nchini na kuokoa fedha zinazotumika kuagiza mafuta ya kula.


Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 4 Novemba 2021 wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania leo tarehe 4 Novemba 2021 Jijini Dar es salaam.


Amesema kuwa Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji na tija ya mazao ya mafuta.


Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kuwapatia vyombo ya usafiri maafisa ugani ikiwemo kununua pikipiki 1,500, vifaa maalum vya kupimia udongo (Soil Test Kits), visanduku vya ugani (Extention Kits), simu janja na kuwezesha  uanzishaji wa mashamba ya mfano kwa kila afisa ugani na kutoa mafunzo rejea.


Amesema kuwa huduma hizo zitawezeshwa kwa kuwa Wizara imeongeza bajeti ya Kuimairisha huduma za ugani kutoka Shilingi milioni 603 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.5 mwaka 2021/2022. Katika utekelezaji wa mpango huo, Wizara imechagua Mikoa mitatu ya Kielelezo ambayo ni Singida, Dodoma na Simiyu yenye fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususan alizeti na pamba.


Waziri Mkenda amesema kuwa Katika mwaka 2021/2022 Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) kutoka Shilingi bilioni 7.35 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.63 mwaka 2021/2022. Vilevile, bajeti ya Wakala wa Mbegu wa Taifa (ASA) kutoka bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 10.58 mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za mazao ya mafuta. 


Vilevile Amesema kuwa Wizara ya kilimo itaendelea kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya pamoja (block farming) katika mikoa inayozalisha mazao ya mafuta kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo mbegu bora, mbolea, viuatilifu na zana bora za kilimo pamoja na mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima. Aidha, Serikali itaimarisha kilimo cha mkataba kwa mazao ya mafuta kwa lengo la kuwa na uhakika wa masoko.


Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuondoa vikwazo vya kisera na kisheria ili kuhamasisha uwekezaji. Maeneo ambayo tumeanza kuyafanyia kazi ni mfumo wa upatikanaji wa mitaji katika sekta ya kilimo na masuala ya kikodi kwenye mazao ya mafuta” Amekaririwa Waziri Mkenda


Amesema kuwa Tanzania ilikuwa ikitekeleza Mkakati wa Kuendeleza Zao la Alizeti kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2020. Malengo mahsusi yaliyoainishwa kwenye Mkakati huo ni pamoja na kuimarisha utafiti wa mbegu bora na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya alizeti.


Ameyataja matokeo yaliyopatikana kutokana na mkakati huo kuwa ni pamoja na Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imesafisha (purification) mbegu bora ya alizeti aina ya Record ili kuongeza uzalishaji na tija; pamoja na kuidhinisha matumizi ya mbegu bora 11 ambazo ni TARI-ILO2019, TARI-NA2019, Aguara4, Aguara6, Hysun33, Supersun64, Supersun66, Michel, Ancilla, Archeo na Soleado.


MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com