METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 16, 2021

MADAKTARI BINGWA WA MAGONJWA WAPIGA KAMBI YA SIKU TANO (5) MWANZA


Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg, Ngusa Samike

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Sekouture Dkt. Bahati Peter Msaki

Wananchi waliojitokeza

Mwananchi akipatiwa huduma.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekouture imezindua kambi ya siku tano(5) iliyoanza Novemba 15 hadi Novemba 19 mwaka huu inayohusisha madaktari Bingwa wa magonjwa mbalimbali hapa Nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg, Ngusa Samike  aliupongeza uongozi wa hospitali na madaktari kuja na mpango Mkakati wa kuhakikisha wanawafikia wananchi wengi.

Alisema kuna changamoto kubwa sana kuwapata madaktari Bingwa, hivyo ili kuwafikia wananchi wengi wameona kuna haja ya kuanzisha kambi huku akibainisha kwamba wataalamu wote wamegharamiwa na serikali kupitia mapato ya serikali.

Sambamba na hilo aliwapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wote ambao wanashiriki kutoa huduma katika kipindi chote cha uwepo wa Kambi hiyo, akisema kwamba ni moyo wa kujitolea ambao umesukumwa na moyo wa dhati wa kuhudumia wananchi.

Akizungumzia maboresho ya hospitali hiyo alisema wako katika ukamilishaji wa ujenzi wa wodi ya mama na mtoto lenye uwezo wa kubeba vitanda 261inayotarajia kukamilika mapema mwakani.

“Lakini pia tutakuwa na  utoaji wa huduma ya kipimo cha  t-scan, pia tunakamilisha ufungaji wa mashine ya kusafisha figo, uwekaji wa mfumo wa kuzalisha hewa ya oxygen na mwaka ujao wa fedha tunatarajia kujenga jengo jingine la kisasa kwa ajili ya wagonjwa wa nje na dharula,” alisema Samike

Aidha kuhusu chanjo ya Covid 19 alisema Hospitali ilipokea chanjo  ya  Johnson &Johnson  na dozi 3050 na uchanjaji ulianza tarehe 3 Agosti, 2021 na kupitia uhamasishaji,  wananchi walijitokeza na kupokea chanjo hiyo.

Sambamba na hilo aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza katika hizi siku tano kupata vipimo vya magonjwa mbalimbali huku akiuomba uongozi isiwe mwisho kuweka kambi za namna hiyo.

“Tunashukuru sana uongozi wa hospitali kwa kutoa huduma hii  na niuombe uongozi hii isiwe mwisho angalau kila  baada ya muda fulani mfanye jambo kama hili  lakini pia wananchi mjitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuja kupata vipimo vya magonjwa mablimbali kwani madaktari hawa kuwapata uwa ni kazi sana,” alisema Samike

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Sekouture na Daktari Bingwa wa Watoto Dkt. Bahati Peter Msaki alisema huduma zitakazotolewa kwa siku tano ni madaktari bingwa wa watoto, akina mama, upasuaji na magonjwa ya ndani.

Alisema lengo la kambi hiyo ni kupeleka huduma karibu na  wananchi kwa urahisi zaidi na kwa kupunguza gharama ambapo kumuona daktari Bingwa itakuwa ni nusu ya gharama halisi ambazo mwananchi angetakiwa kulipia.

“Hospitali imefanya maboresho mbalimbali ikiwemo kununua mashine za maabara za kutosha , kununuliwa kwa mashine kubwa ya mionzi, ununuzi wa dawa za kutosha na lengo ni kutoa huduma bora kwa gharama nafuu hivyo wananchi waje kwa wingi katika kipindi hiki kwa ajili ya kuangalia afya zao,” alisema Dkt Bahati

Aliongeza kuwa kumuona Daktari Bingwa itakuwa ni shilingi elfu kumi (10,000) tu ila kwa vipimo kama shinikizo la damu, uzito, kisukari, homa ya ini, saratani ya matiti na kizazi vipimo vyake vitatolewa bure.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata vipimo katika kambi hiyo wameushukuru uongozi wa hospitali na serikali kwa ujumla kuona haja ya kufanya hivyo kwani gharama za kuwaona madaktari bingwa huwa ni kubwa na baadhi yao hushidwa kuzimudu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com