Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ameutaka
uongozi wa chama cha wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa na Mkuu wa kitengo
cha uchumi na uzalishaji ili kuongea na
Wakurugenzi wa Halmashauri kwa
lengo la kuwatafutia maeneo ambayo watakuwa wakizalisha na kuuzia bidhaa zao.
Maagizo hayo yametolewa Oktoba 19, 2021 Jijini Mwanza na
Emil Kasagara Katibu Tawala Msaidizi na Mkuu wa kitengo cha uchumi na
uzalishaji cha Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi
Robert Gabriel aliyekuwa mgeni rasmi wakati akizungumza na wafanyabiashara wanawake
na kusema Serikali inatambua na
kuthamini mchango mkubwa wa uchangiaji wa uchumi unaofanywa na wanawake kupitia
shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na wao wako bega kwa bega katika
kusaidia juhudi hizo.
“Nimesikia katika risala yenu mkitaja kukosekana kwa eneo la
kuzalishia na kufanyia biashara kuwa ni changamoto kubwa kwenu kushindwa
kufikia malengo , kimsingi Mkoa hauna maeneo, maeneo yote yapo chini ya
Halmashauri hivyo namuelekeza Katibu tawala Mkoa na Mkuu wa kitengo cha uchumi
na uzalishaji kukutana nanyi ili muombe kukutana na wakurugenzi wa halmashauri
wawasaidie kupata hayo maeneo.” Amesema
Aidha amewataka kuandaa andiko ambalo litaelezea eneo
wanalotaka, ukubwa wa eneo, shughuli watakazofanya katika eneo hilo ili iwe
rahisi kwa Wakurugenzi kuwapa maeneo ambayo yataenda sambamba na mahitaji yao.
Kuhusu kukosa soko la bidhaa zao amewataka wafanyabiashara
hao kuzalisha bidhaa zenye ubora kwani
ndo njia pekee za kuwashawishi watanzania kupenda bidhaa zinazozalishwa nchini
na pia zitaleta ushindani katika soko la bidhaa.
“Mmesema bidhaa zenu hazinunuliwi na Watanzania, labda
niwaambie kitu hakuna mtu ambaye atapenda kununua bidhaa ambayo haina ubora
lakini mkiwa na bidhaa bora mtauza kwani kuna msemo unaosema kizuri chajiuza na
kibaya chajitembeza hivyo mkizingatia vitu vyote ikiwemo bidhaa kuwa na
viwango, kupitishwa na mamlaka zikiwemo TBS, TMDA kuwa na barcode nawahakikishia zitauzwa tu.”
Amesema
Pia amewataka wanawake hao, kutumia chama chao kwa ajili ya
kuziendea taasisi za kifedha kukopa ili kuendeshea shughuli zao pamoja na zile
asilimia 4 ambazo zinazotolewa na
halmashauri zisizo na riba yoyote kwa wanawake.
“Kila Halmashauri imetenga asilimia 10 za fedha kwa ajili ya
makundi ya wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4 na watu wenye ulemavu
asilimia 2 kwa kutumia mikopo ya fedha hizi mnaweza kuongeza mitaji ya biashara
zenu na mkumbuke kuwa fedha hizi hazina riba changamkieni fursa hii.” Amesema
Akizungumza wakati wa kongamano hilo mwenyekiti wa chama
hicho Mkoani Mwanza Bi Fausta Ntara amesema chama mpaka sasa kinawanachama 1070
pamoja na tawi moja lililopo Wilayani Magu ambalo limefunguliwa mwaka huu
lakini wanamalengo ya kufungua matawi katika kila wilaya ili kuwafikia wanawake
popote pale walipo na wao wafikiwe na
fursa mbalimbali.
Katika Risala yao iliyosomwa na katibu msaidizi wa chama
hicho Mkoani hapa Bi Jane Simon Ndeto imesema lengo mahususi la TWCC ni
kuwawezesha wanawake wajasiliamali kupambana kikamilifu katika kukuza uchumi,
kuwawezesha wanawake kuona fursa mbalimbali za kibiashara na kuzitumia kwa
lengo la kuwa na biashara endelevu zenye kuleta tija kwa wanawake na kuwajengea
uwezo wa kujiamini katika kusimamia biashara zao.
Ameyataja mafanikio waliyoyapata ikiwemo kuongezeka kwa
wanachama pamoja na changamoto zikiwemo ukosefu wa maeneo ya kuzalishia na
kuuzia bidhaa, masharti upatikanaji wa vibali vya kuzalisha bidhaa kutoka TBS,
TMDA, BARCORD, OSHA kodi na tozo kuzidi,
mitaji midogo, masharti magumu ya kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha
pamoja na watanzania kutopenda bidhaa zinazozalishwa nchini.
Aidha wameiomba serikali kupunguza masharti ya upatikanaji
wa bidhaa, kupunguzwa kwa kodi na tozo
zipunguzwe pamoja na kupatiwa eneo ambalo watajenga jengo la kuzalisha bidhaa
na masoko ya kuuzia bidhaa pamoja na kuomba fedha za mradi wa vifungashio kwa
ajili ya wajasiliamali wote Mkoani Mwanza na Mikoa ya jirani.
Kupitia kongamano hilo wanawake hao walipewa elimu juu ya
faida mbalimbali za kuwa na barcode kwenye bidhaa zao kutoka GS1 Tanzania
ambapo kupitia afisa masoko wao Shabani Mkongoti amesema mbali na kuongeza
thamani ya bidhaa barcode pia hutambulisha bidhaa kimataifa na kupata mrejesho
wa bidhaa sokoni pamoja na kuongeza wigo wa biashara.
Amesema barcode humuwezesha mfanyabiashara kufahamu kifungashio gani huwezesha bidhaa kuuzwa Zaidi sokoni, hulaisiha mfumo wa mauzo na hutumiwa dunia nzima ,huleta faida kwa nchi, kwa wajasiliamali na muuzaji wa rejareja na kwa nchi zinazoendelea wanunuzi hutumia barcode kuitambua bidhaa ilivyotengenezwa mpaka gharama yake.
0 comments:
Post a Comment