METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 18, 2021

WAZIRI WA KILIMO PROF MKENDA ATEMBELEA KAMPUNI YA MBOLEA YARA JIJINI DAR ES SALAAM

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua upatikanaji wa mbolea wakati alipotembelea kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania yenye maskani yake Kurasini Jijini Dar es salaam, leo tarehe 18 Septemba 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua maghala ya kuhifadhia mbolea ya kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania katika eneo la Kurasini Jijini Dar es salaam, leo tarehe 18 Septemba 2021.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya YARA Ndg Winstone Odhiambo akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda mara baada ya kukagua maghala ya kuhifadhia mbolea ya kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania katika eneo la Kurasini Jijini Dar es salaam, leo tarehe 18 Septemba 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo mara baada ya kukagua maghala ya kuhifadhia mbolea ya kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania katika eneo la Kurasini Jijini Dar es salaam, leo tarehe 18 Septemba 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akikagua hali ya upatikanaji wa mbolea ya kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania katika eneo la Kurasini Jijini Dar es salaam, leo tarehe 18 Septemba 2021.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 18 Septemba 2021 ametembelea na kufanya mazungumzo na Ndg Odhiambo Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mbolea ya YARA Tanzania yenye maskani yake Kurasini Jijini Dar es salaam.

Pamoja na kujionea shehena kubwa ya mbolea Waziri Mkenda ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji mkubwa iliyofanya nchini na kuwarahisishia upatikanaji wa mbolea wakulima kote nchini.

Amesema kuwa kampuni hiyo imeendelea kujipatia faida kubwa ya uuzaji wa mbolea tangu ilipoanza kufanya biashara zake nchini, hivyo wakati huu ambao kumekuwa na changamoto ya gharama kubwa kwa wakulima wanapaswa kuona uwezekano wa kupunguza bei.

Prof Mkenda amezishukuru kampuni za mbolea YARA pamoja na OCP kwa kufanya biashara kwa ufasaha mkubwa wa mbolea ambazo zimekuwa zikifika kwa wakati na kuuzwa kwa wakulima.

“Kuna watu bado hawafahamu wakiona bei ya mbolea imepanda wanadhani Wizara ya Kilimo au serikali imepandisha bei jambo ambalo sio kweli kwani bei ya mbolea imepanda katika soko la Dunia” Amekaririwa Waziri Mkenda

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya YARA Ndg Winstone Odhiambo ameomba kupewa muda wa siku chache ili afanye mazungumzo na viongozi wakuu wa kampuni hiyo ili kuona uwezekano wa kupunguza gharama kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Tanzania.

Odhiambo amesema kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuimarisha usafiri wa reli kwani kwa kusafirisha mbolea kwenda mikoani kwa kutumia treni kumepunguza gharama za usafirishaji.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com