METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 28, 2015

ULIPO MOYO WA MTU NDIPO NA HAZINA YAKE ILIPO.!



Na Malisa GJ,

Unataka kufanikiwa? Fanya kile unachokipenda, na ukifanye kwa moyo (bidii). Kama unapenda utangazaji usisomee Udaktari kisa tu unafaulu Biology darasani. Somea utangazaji. Utafanya vizuri zaidi. Watu wengi waliofanikiwa duniani wamefanya vitu wanavyovipenda.

Kama umesomea fani usiyoipenda kisa tu umeambiwa ina kazi za haraka haraka au ina hela umepotea. Siku ukimaliza kusoma usipate kazi au ukapata kazi lakini isiwe na hela kama ulivyotarajia UTAJILAUMU sana.

UFANYE NINI? Kama umesomea kitu usichokipenda achana nacho, fanya kile unachokipenda na kinachokupa amani. Kama umesomea Sheria wakati moyo wako upo kwenye biashara ni ngumu sana kufanikiwa kupitia sheria. Achana na sheria, fanya biashara.

Mark Zukerberg mmiliki wa mtandao wa Facebook alikuwa anasomea shahada ya Uhandisi wa Computer akakwazana na mwalimu wake. Mwalimu alimlazimisha kukariri "Laws" za Pysics za kina Gallileo Gallilei wengineo, lakini Mark hakutaka kukariri vitu vya watu, alitaka kubuni vya kwake.

Alipoona hawaelewani na mwalimu akaacha shule akaenda kufanya kitu alichokipenda na leo amefanikiwa sana. Leo Mark yupo kwenye list ya matajiri 10 wa dunia.

Mwanamuziki wa Congo aitwae Antoine Christopher Agbepa Mumba maarufu kama "Koffi Olomide" alisomea shahada ya Uchumi. Akafanya kazi kidogo bank. Lakini akaona anafanya kitu asichokipenda, maana moyo wake wote ulikuwa kwenye muziki. Akaachana na bank akaingia kwenye muziki na amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Mustapha Hassanali alipenda mambo ya mitindo (fashion) tangu akiwa mtoto. Lakini wazazi wake walitaka awe daktari. Hassanali akalazimika kusomea kitu asichokipenda ili tu awaridhishe wazazi. Akasoma kwa bidii hadi akafaulu kujiunga na chuo kikuu cha sayansi ya tiba Muhimbili kusomea udaktari.

Alipomaliza miaka yake mitano ya udaktari na kugraduste akakataa kwenda kufanya internship maana udaktari sio kitu alichokipenda. Akaachana na udaktari akaingia kwenye mitindo, na amefanikiwa sana kupitia mitindo. Kwa sasa ni miongoni mwa wanamitindo wa kitanzania wanaokubalika sana nje ya mipaka hadi nchi za Ulaya, Asia na Marekani.

Je unamfahamu Doctor Mitch Egwang?? Huyu ni Presenter anayelipwa ghali zaidi kuliko wote barani Afrika. Ndiye amekuwa akihost Tusker Project Fame kwa muda mrefu sasa. Unajua kwanini anaitwa "doctor?" Au unadhani ni swaga kama za kina "Doctor Cheni?"

Dr.Egwang ni daktari halisi wa mifugo (qualified veterinary doctor). Amehitimu shahada yake ya udaktari wa mifugo chuo kikuu Makerere. Lakini tangu wakati anasoma shule ya msingi moyo wake ulikuwa kwenye utangazaji (TV Presenter).

Na alipomaliza elimu ya sekondari akataka kujiunga na chuo kikuu alitaka kusoma Journalism/Mass Communication au taaluma nyingine inayohusiana na kitu alichokipenda. Lakini wazazi wake walimkataza kwa sababu mbili.

Mosi eti alikuwa amefaulu vzr masomo ya "Sayansi" hivyo haingekuwa vizuri kwenda kusomea Utangazaji wakati alikua na "A" ya Biology na "A" ya Chemistry. Pili wazazi wake walimwambia Mambo ya kutangaza ni kazi za "kike" hivyo hazimfai yeye. So akaamua kuwasikiliza wazazi na kwenda kusomea Udaktari wa mifugo kwa shingo upande maana si kitu alichokuwa anakipenda.

Alipohitimu akaamua kufuata moyo wake, akaweka kando taaluma ya mifugo na akajielekeza kwenye utangazaji. Na kwa sasa ndiye Presenter anayelipwa ghali zaidi katika bara la Afrika. Inakadiriwa wastani wa kipato chake kwa mwezi ni dola elfu hamsini, karibia shilingi milioni 90 za kitanzania. So kila mwezi Dr.Egwang anatengeneza milioni 90.

Wabunge wa Tanzania wanalipwa mshahara wa mil 3.5 kwa mwezi ukiondoa posho. Hii ni sawa na kusema "daktari wa mifugo" Dr.Egwang anaweza kulipa mishahara wabunge 30 wa Tanzania kila mwezi kupitia kazi zake za uPresenter na uMC.

Lakini mafanikio yote haya Dr.Egwang angeyaona kama ndoto kama angesikiliza wazazi wake na aamue kufanya kazi ya udaktari wa mifugo. Yamkini leo angekuwa anatibu ng'ombe, punda na kuku zenye videri kule kwa Mbarara, Uganda. Lakini ALIACHANA na kitu alichokisomea ili afanye kile alichokipenda, na AMEFANIKIWA.

List ya watu "waliotupa" Career zao na kufanya vitu wanavyovipenda ni ndefu lakini kwa leo tuishie hapa. Sasa jiulize je, wewe bado unafanya kitu usichokipenda kisa tu umekisomea? Bado wewe ni mtumwa wa taaluma yako?

Ulipenda sana kuwa mwanasheria lakini wazazi wako wamelazimisha usomee uhasibu, sahau kuhusu mafanikio. Ulipenda sana uwe mwalimu na unaenjoy ukifundisha lakini wazazi wako, ndugu au jamaa wamelazimisha umesomea Engineering, sahau kuhusu mafanikio.

Biblia inasema "ulipo moyo wa mtu ndipo na hazina yake ilipo". Maana yake ni kwamba kama moyo wako upo kwenye sheria it means mafanikio yako/hazina yako ipo kwenye sheria pia.

Sasa wewe moyo wako upo kwenye biashara lakini umesomea Ualimu huwezi kuipata hazina yako hadi urudi kule moyo wako ulipo (kwenye biashara). Hii ni kanuni ya kiroho.!

Sasa je, wewe bado unafanya usichokipenda? ACHANA nacho leo tafuta kile unachokipenda ukifanye. Unaogopa kuacha kisa umekisomea? Hayo ni mawazo duni. Hakuna watu waliofanikiwa kwa sababu ya kufanya vitu walivyovisomea, wapo waliofanikiwa kwa sababu ya kufanya vitu walivyovipenda.

Ingekuwa mtu anafanikiwa kwa kufanya alichokisomea basi maprofesa wote duniani wangekuwa "mabilionea" maana wao ndio wamesomea taaluma zao kwa viwango vya juu kabisa.
Kama unafanya kitu unachokipenda una nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kuliko anayefanya asichopenda hata kama amekisomea.

Ieleweke kwamba "sidiscourage" taaluma za watu, wala sipingi watu kusomea taaluma mbalimbali. Hojo yangu ni kuwa ukitaka kusomea kitu basi somea kile unachokipenda. Utafanikiwa zaidi kuliko kusomea kitu usichokipenda.

Jiulize ulipomaliza kidato cha 4 kwenda cha tano, combination uliyosoma ulichagua wewe mwenyewe kwa kuipenda au ulichaguliwa. Wewe ulitaka kusoma HKl au HGL ukaambiwa achana na "kombi za kike" nenda ECA ndio mpango mzima. Ukaenda ECA kwa pressure ya ndugu, jamaa na marafiki. Wewe kufanikiwa ni ngumu sana.

Ulipomaliza form six ukaenda chuo je "course" uliyoisomea ndio ilikua chaguo lako? Ndiyo uliyoipenda? Ulikua na ndoto za kuwa Mwanasheria na unaipenda sheria kutoka moyoni lakini ukasomea "digrii ya Human Resource" kisa uliambiwa HR ina hela. Wewe kufanikiwa ni ngumu sana.

Au ulikua na mpango wa kusomea "Sociology" lakini TCU wakakupanga "Mass Communication" na ukasoma tu Mass Com kisa TCU wamekupanga. Wewe kufanikiwa ni ngumu sana.
Unakutana na mtu yupo chuo kikuu mwaka wa tatu anasomea "Hot Culture" pale SUA lakini haipendi kabisa maana alitaka awe "Nesi". Unamuuliza sasa kama unapenda kuwa Nesi mbona unasomea "Hot Culture" anakujibu kinyonge "Basi tu TCU walinipangia"

Sikiliza nikuambie kitu. Ukitaka kufanikiwa TCU hawapaswi kuamua hatma ya maisha yako. Ndugu zako hawapaswi kuamua hatma ya maisha yako. Marafiki zako pia hawapaswi. Hatma ya maisha yako iko mikononi mwako mwenyewe. Fanya kile unachokipenda na unahisi una amani kukifanya utafanikiwa.

Je unahisi umechelewa. Kama umesomea Ualimu na ndoto zako zilikuwa uwe Mhasibu unadhani umechelewa? Au ulitaka uwe TV presenter lakini TCU 'wakaamua' usome LLB, je unahisi umechelewa kwa kuwa umeshahitimu "digrii ya LLB?"
Jibu ni kwamba HUJACHELEWA. Mathalani bado una pumzi na nguvu hujachelewa. Achana na hicho ulichokisomea kama hakikupi amani fanya kile unachokipenda.

Namkumbuka rafiki yangu mmoja aliyekuwa anapenda sana kufanya biashara tangu akiwa mtoto. Tangu shule ya msingi alikuwa akinunua saa mjini, wakati ule tunaziita saa za "mkonyezo" kisha anakuja kutuuzia shuleni.

Alikua akinunua saa moja sh.500 anakuja kutuuzia sh.800. Anapata faida ya sh.300 kwa saa moja, akiuza saa 10 kwa wiki ana faida ya sh.3000. Hazikuwa hela ndogo kwa mtoto wa shule ya msingi kutengeneza sh.3000 kwa wiki by then.
Jamaa hakuwa serious sana darasani lakini alikuwa na akili za kuzaliwa. Washamba tunaziita "akili za nature"
Kwa hiyo hakuwa na mpango wa kusoma sana. Mpango wake ulikua kufanya biashara lakini kwa kuwa alifaulu ikabidi aendelee. So akaenda sekondari huku anafanya biashara na kukuza mtaji wake. Alipofika form six alitaka iwe ndio mwisho wa elimu, ili ajikite zaidi kwenye biashara. Lakini" unfortunately" akapata "division one".

Alipowaambia wazazi kuwa hana mpango wa kuendelea bali anataka kufanya biashara wakamuona "chizi". Baba yake akamwambia "hapa mtaani wazee wenzangu wote wana watoto wenye digrii. Tukikaa nao kunywa mbege mimi nitasemaje wakati wewe ndio mwanangu wa kwanza.!! Hebu nenda kaniletee digrii kwanza halafu hayo mengine badae"

Jamaa akaenda chuoni akasoma digrii yake ya sheria. Lakini wakati huohuo anafanya biashara. Mara kaenda Zanzibar kuchukua mzigo, mara Uganda ili mradi tu biashara ipo "damuni". Hakuwa serious sana na masomo lakini alimaliza.

Akiwa mwaka wa tatu tayari alikua anamiliki daladala, duka la vipodozi, na "barber shop" ya kisasa.
Baada ya "kugraduate" alichukua vyeti vyake vyote akampelekea mzee wake kule Moshi akamwambia "baba ile kazi uliyonituma kuifanya nimeimaliza. Degree yako hii hapa. Sasa unaweza kukaa kwa amani na wazee wenzako mkinywa mbege huku ukijisifu una mtoto mwenye degree"
Akarudi kuendelea na biashara. Majuzi tulikutana Mafinga, mimi nikielekea Njombe, yeye akiwa anapakia mbao kupeleka Nairobi. Anasema akijaza lorry moja anatumia kama milioni 45 hadi 50 pamoja na kodi. Zikifika Nairobi anapata milioni 70 hadi 75. Maana yake ni kuwa anatengeneza faida ya milioni 20 hadi 25 kwa "trip" moja. Sasa hata trip moja ikitumia mwezi mzima si mbaya, maana ni sawa na kutengeneza mil.25 kwa mwezi.

Licha ya hapo ana-supply nyama kwenye shule kadhaa za sekondari hapa Dar, anamiliki stationery pale Mabibo hostel, na duka la vipodozi maeneo ya Ubungo. Daladala aliuza anasema biashara ya magari ni "pasua kichwa"

Kwa umri wa miaka 30 alionao naweza kusema amefanikiwa kwa kuwa alichagua kufanya kitu alichokipenda. Angetaka kufanya kazi za sheria kisa ndio taaluma aliyoisomea bila shaka leo angekua "Hakimu wa mahakama ya mwanzo kule Mikindani, Mtwara".

Narudia kuwakumbusha kuwa "ulipo moyo wa mtu ndipo na hazina yake ilipo". Je wewe moyo wako uko wapi? Kama upo kwenye Uhandisi (Engineering) usisomee Ualimu (Education) ili tu upate mkopo. Kama moyo wako upo kwenye Sheria (LLB) usisomee Uandishi wa habari kisa tu TCU wamekupanga. Fuata moyo wako. Nafasi unayo, anza sasa.!

Malisa GJ || Your Partner In Critical Thinking.!
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com