Waziri wa Kilimo Mhe Prof.
Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TAHA Dkt
Jacqueline Mkindi walipotembelea shamba la kampuni ya uzalishaji wa ndizi
pamoja na karanga aina ya Macademia ya Macjaro Ltd iliyopo eneo la Machame katika
Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya kikazi ya kamati ya kudumu
ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Tarehe 14 Agosti 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe Dkt. Christine Ishengoma
ameipongeza Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi Kilele inayojihusisha na ulimaji
wa mbogamboga, maua na mazao ya bustani TAHA kwa uwekezaji mzuri nchini.
Dkt Ishengoma ametoa pongezi
hizo tarehe 14 Agosti 2021 mara baada ya kutembelea na kukagua shamba la
kampuni ya African Vegetable Limited, Shamba la Macjaro Limited lililopo
Machame Wilayani Hai na Shamba la Vasso Agroventures Ltd lililopo katika kijiji
cha Mkoringa kata ya Kibosho Wilaya ya Moshi Vijijini.
Mhe Ishengoma ameahidi
kuzisimamia na kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo
nchini zinatatuliwa na serikali kupitia Wizara ya kilimo ili kuongeza uwekezaji
na ajira kwa watanzania wengi.
Akizungumza katika ziara hiyo
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa sekta ya mbogamboga, maua
na mazao ya bustani haina changamoto ya soko hivyo wananchi wanapaswa kuuona
umuhimu wa kuwekeza katika sekta hiyo.
Amesema kuwa sehemu kubwa ya
mazao mengi nchini wakulima hulima bila kujua soko lilipo lakini katika sekta
hiyo mkulima anaweza kulima huku akiwa na uhakika wa soko la ndani nan je ya
nchi.
Amesema kuwa serikali
inatambua umuhimu wa zao la ndizi hivyo tayari imejipanga kufanya mkutano
maalumu kwa ajili ya kuweka mikakati ya kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na
kufungua maabara ya utafiti ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi Kilele inayojihusisha na ulimaji wa mbogamboga, maua na
mazao ya bustani-TAHA Dkt Jacqueline Mkindi amesema kuwa sekta hiyo imeendelea
kupata ushirikiano madhubuti kutoka serikalini jambo ambalo linaimarisha
uhusiano wa kiutendaji.
Amesema kuwa ziara hiyo ya
kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imetoa fursa ya kuimarisha
sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji utakaotoa fursa kubwa ya ajira
kwa vijana ikiwa ni pamoja na kuimarisha kipato cha wananchi.
Amesema Tanzania ina ardhi
yenye rutuba nzuri, uwepo wa maji ya kutosha hivyo matarajio yake ni kujipanga
vizuri kwenye mifumo na miundombinu ya kufikia masoko ili kutengeneza mapato kwa
mwaka kwa zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 6.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment