Na Mathias Canal, Rombo-Kilimanjaro
Mamia ya wananchi wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na
kwingineko nchini wamejitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la
Rombo na kushika wadhifa mkubwa akihudumu wakati huo kama waziri wa fedha, Mhe
Basil Pesambili Mramba.
Katika shughuli hiyo ya kuaga mwili huo iliyofanyika katika
viwanja vya sabasaba vilivyopo katika Halamshauri ya wilaya ya Rombo kwa niaba
ya serikali, iliongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda
aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan.
Mhe Mramba ambaye alifariki Agosti 17, mwaka huu katika
hospitali ya Regency iliyopo mkoani Dar es salam ameagwa katika uwanja wa
sabasaba na kisha kuzikwa kijijini kwake Shimbi wilayani Rombo.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Samia,
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ambaye amesema Taifa litamkumba Basil
Mramba kwa uzalendo na juhudi zake alizozifanya wakati akiwa katika nyadhifa
mbalimbali za uwaziri serikali na kusema ameacha alama kubwa kwa Taifa
inayopaswa kutambuliwa ipasavyo.
Waziri Mkenda amesema kuwa, Mramba ameacha alama ambazo hazitafutika kamwe katika wilaya ya Rombo hasa katika suala la barabara na kilimo cha ndizi na maparachichi ambacho ndio uchumi mkubwa na tegemezi kwa wananchi wa wilaya hiyo.
"Wananchi wa Rombo kamwe hatutamsahau Mramba kwa mambo makubwa aliyoyafanya wakati wa ubunge wake,wakati anaingia kwenye ubunge kwa mara ya kwanza Rombo ilikuwa na shule nne pekee za Sekondari na mpaka anaondoka kwenye nafasi hii ya ubunge alicha shule zaidi ya 40 kutokana upambanaji wake," Amekaririwa Profesa Mkenda
Waziri huyo wa Kilimo Mhe Profesa Mkenda amewaahidi wananchi wa
Jimbo hilo kuwa ataendeleza yale yote ambayo Mramba alitamani kuyakamilisha
lakini hayakukamilika wakati alipouwa madarakani.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro, Ndg
Patrick Boisafi amesema kifo cha Mramba ni pigo kubwa kwa wanachi na wakazi wa
Rombo na Taifa kwa ujumla kwani alikuwa ni mtu aliyetumikia Taifa kwa upendo na
kulipenda jimbo lake.
"Mramba ameacha alama hapa Rombo na Taifa kwa ujumla,
maisha yake yanajieleza na alifanya kazi kubwa kwenye nchi hii na sisi sote ni
mashahidi, aliipenda Rombo na Kilimanjaro kwa ujumla tuna cha kujifunza
kupitia kwake, alitumia nafasi aliyopewa na serikali kuwatumikia wananchi
wake," Amesema Boisafi
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi, Mwakilishi wa Askofu wa
jimbo katoliki la moshi, Padre Deogratius Matiika amesema Mramba ameandika
historia katika jimbo hilo na kwa kanisa katoliki na kwamba atakumbukwa kwa
mengi kwani alikuwa ni kimbilio la wengi.
"Tutaendelea kumuenzi ndugu yetu Mramba amekuwa ni mti
mzuri uliozaa matunda kwani alimpenda Mungu na alimtumikia ipasavyo, alishiriki
nasi katika maeneo mbalimbali pale ambapo kulikuwa na msaada kanisani
alitusaidia, ameandika historia ambayo haitafutika Kilimanjaro, hakuna
anayeweza kupinga hili kwamba aliweka historia wilaya ya Rombo,"
Amesisitiza Padre Matiika
Mramba alihudumu katika nyadhifa mbalimbali za uwaziri ikiwemo
Waziri wa Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia alikuwa mwanzilishi
wa viwanda vidogo vidogo nchini (SIDO)
MWISHO
0 comments:
Post a Comment