Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf
Mkenda (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano mkuu wa wadau wa tasnia
ya korosho katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania tawi la Mtwara leo
tarehe 27 Agosti 2021. (Picha Zote na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Mb) ameielekeza Bodi ya Korosho kuruhusu usafirishaji wa korosho ghafi nchini kuanzia msimu huu wa 2021/2022 kufanyika ufanyike kwa saa 24 badala ya saa 12 kama ilivyokuwa katika misimu ya nyuma ili kulinda ubora wa zao, kuongeza kasi ya usafirishaji wa korosho kupitia Bandari ya Mtwara na kuongeza ushindani wa bei ya korosho kwenye minada.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo
leo tarehe 27 Agosti 2021 wakati akifungua mkutano mkuu wa wadau wa tasnia ya
korosho katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania tawi la Mtwara
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha sekta
ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na mfumo thabiti wa
upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo ambapo kwa sasa Serikali imeruhusu
waagizaji wa pembejeo waagize kadri ya mahitaji ya wakulima badala ya mfumo wa
ununuzi wa pamoja ambao ulikuwa na mapungufu kadhaa.
Waziri Mkenda amesema kuwa Katika zao la korosho
hivi sasa wakulima wanapata pembejeo kupitia Vyama vya Ushirika na hivyo
kuwezesha kufikia malengo ya uanzishwaji wa vyama hivyo.
“Tunaposema kazi iendelee, tunamaanisha kila mmoja aendelee kutimiza wajibu
wake ipasavyo. Mkulima alime kwa
kuzingatia stadi za kilimo; Mnunuzi
azingatie taratibu za ununuzi tulizojiwekea; Kiongozi wa Ushirika aendeshe Ushirika kwa uadilifu mkubwa na Msimamizi wa zao (Bodi), awe nahodha wetu
kwenye kuimarisha zao husika kwa kuishauri vema Serikali kuhusu namna ya
kwenda mbali Zaidi” Amekaririwa Waziri Mkenda na kuongeza kuwa
Viongozi wa Serikali, Mkoa na Wilaya kufuatilia
mwenendo wa biashara ya korosho na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kuwa mkulima
anapata anachostahili.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Changamoto kubwa
inayokabiliwa katika sekta ya kilimo nchini ni kupungua kwa tija, ubora na
uzalishaji wa mazao hapa nchini ikiwa ni pamoja na zao la korosho.
“Changamoto hii inajidhihirisha kwenye
mwenendo wa masoko ya mazao yetu hapa nchini. Njia mojawapo ya kukabiliana na
changamoto hii ni kuzingatia kanuni za kilimo bora kama inavyoshauriwa na
maafisa ugani wetu kutokana na utafiti wa teknolojia za kisasa za kilimo kutoka
kwenye vituo vyetu vya utafiti (TARI)” Amekaririwa Prof Mkenda
Aidha, Prof. Mkenda alieleza kwamba mazao ya
biashara yanayotozwa Export Levy ni Korosho peke yake pamoja na biashara ya
ngozi ghafi. Hivyo Wizara itaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba Export Levy
katika zao la korosho ni lazima irudi ili kusaidia maendele ya zao hilo kama
ambavyo ilikuwa imekusudiwa wakati wa uanzishwaji wa tozo hiyo.
Ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya
Korosho kuhakikisha wanaandaa mpango wa matuzi ya fedha hizo katika kuendeleza
zao la korosho.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) Mhe George Mkuchika amesema kuwa mkutano huo una
umuhimu mkubwa kwani Korosho ni zao linaloiingizia serikali fedha nyingi za
kigeni na kuimarisha uchumi wa nchi na wananchi wote.
Amesema kuwa Waziri wa Kilimo Prof. Adolf
Mkenda ameanza usimamizi wa sekta ya Kilimo kwa weledi mkubwa hivyo ni wajibu
wa kila mshiriki kutoa maoni yake kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi makubwa ya
tasnia ya korosho.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe Jackson Kiswaga ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Kalenga amesema kuwa pamoja na ufanisi wa kazi wa Wizara ya
Kilimo lakini pia inapaswa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na
ambazo ni stahimili ili wakulima wanapozalisha mazao yao waweze kupata faida
pamoja na upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi
ya Korosho Tanzania Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Damian Mwanjile amesema
kuwa Bodi hiyo itafanya kazi kwa karibu na wataalamu wa Bodi ya Korosho ili
kuhakikisha kuwa kusudio la serikali katika kuongeza tija na uzalishaji wa zao
la Korosho nchini unafikiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Dunstan Kyobya akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amewasisitiza wajumbe wa mkutano huo wa wadau wa Korosho kuhakikisha kuwa wanachukua tahadhari zote ikiwa ni pamoja na kunawa mikono na kuvaa barakoa ili kukabiliana na ugonjwa wa UVICO 19.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment