Baadhi ya wakulima wakifuatilia mnada wa mbaazi zinazouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma
CHAMA Kikuu cha Ushirika cha wilaya ya Songea na Namtumbo(Sonamcu Ltd)cha mkoani Ruvuma, kimefanya mnada wa tatu wa zao la mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani huku wakulima wakifurahi bei nzuri inayotolewa na wanunuzi.
Meneja wa Sonamcu Juma Mwanga amesema, Sonamcu imefanya minada mitatu na hadi sasa kilo 1,327,513 zimeuzwa na Sh. Bilioni 1,727,765.879 zimelipwa kwa wakulima.
Amesema, katika mnada wa kwanza uliofanyika tarehe 11 Agosti, jumla ya kilo 41,428 zimeuzwa kwa bei ya Sh.1,280 kwa kilo ambazo zimenunuliwa na Kampuni ya Ginning Afrisian ambayo imelipa Sh. 53,027,840.00 na baada ya tozo ya Sh.57 kwa kilo wakulima wameingiziwa jumla ya Sh.50,666,444.00 kwenye akaunti zao.
Amesema, mnada wa pili umefanyika tarehe 18 Agosti na kilo 406,517 zimeuzwa kwa bei ya Sh. 1,320 kwa kilo moja na kufanya fedha zilizoingia kwa mnada huo kufikia Sh.536,602,440.00.
Mwanga amesema,katika mnada huo makampuni matano yalijitokeza kwa ajili ya kutaka kununua mbaazi,hata hivyo makampuni mawili ya Mohamed Enterprises na Lenic Tanzania Ltd ndiyo yaliyoshinda na kupata fursa ya kununua mbaazi zote zilizoingizwa mnadani.
Kwa mujibu wa Mwanga, katika minada hiyo miwili wanunuzi wamechangia jumla ya Sh.16,126,020.00 kama ushuru kwa Halmashauri na wakulima wamechangia Sh.895,890.00 katika mfuko wa maendeleo kwa Halmashauri ya wilaya.
Mwanga amesema, Chama Kikuu cha Ushirika(Sonamcu Ltd)kimepata jumla ya Sh.6,719,175.00 kama ushuru wa mauzo ya mbaazi kutokana na usimamizi na uratibu wa shughuli nzima za minada katika wilaya ya Namtumbo.
Mbali na Sonamcu,vyama vya Msingi vya Ushirika(Amcos)vimepata jumla ya Sh.15,678,075.00 kutokana na kuuza mbaazi za wanachama wake kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Aidha amesema, katika mnada wa tatu uliofanyika tarehe 25 Agosti, kilo 879,568 zimeuzwa ambapo kampuni ya Lenic Tanzania Ltd imenunua mbaazi zote kwa bei ya Sh. 1,380 kwa kilo moja, na kuwalipa wakulima jumla ya Sh. 1,213,803,840.
Hata hivyo amesema, baada ya tozo ya Sh.57 kwa kilo wakulima wamelipwa Sh. 1,323 na kufanya jumla ya fedha zilizoingia kwenye akaunti za wakulima kutokana na mnada huo kufikia Sh. 1,163,668.
Mkulima wa mbaazi Ziaba Twaibu,ameishukuru Serikali kwa kusimamia vyema mfumo wa stakabadhi ghalani hasa kwa zao la mbaazi ambalo siku za nyuma halikuwa na thamani kutokana na kukosa wanunuzi.
Amesema, mfumo wa kuuza mazao kwa utaratibu wa stakabadhi ghalani licha ya kumwezesha mkulima kupata soko la uhakika, umesaidia kurudisha mahusiano ya familia na kuimarika kwa ndoa nying na kuhaidi kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa msimu ujao.
Mkulima mwingine Hajali Ndimbo amesema, kwa ujumla zao la mbaazi limeleta tija kubwa kwa wakulima na kukomesha vitendo vya dhuluma na wizi vilivyokuwa vinafanywa na wafanyabiashara.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kuendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao yote ya biashara na kuongeza wanunuzi wengi ambao wataleta ushindani wa bei ya mazao.
Mwenyekiti wa Sonamcu Ali Chemka, ametoa wito kwa wakulima ambao hawajapeleka mbaazi zao kwenye maghala, wapeleka ili kuwahi bei na msimu mpya wa kilimo .
Amesema, katika msimu wa mwaka huu hakuna changamoto ya kuchelewa malipo ya wakulima,kwa hiyo ni vyema wakulima wakachangamkia fursa hiyo iliyoletwa na Serikali, badala ya kuuza kwa wafanyabiashara wa mitaani wanaonunua kwa bei ya chini.
Chemka amesema, minada ya mbaazi inayofanywa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani imesaidia kuzuia vitendo vya wizi vinavyofanywa na wafanyabiashara dhidi ya wakulima.
Pia,stakabadhi ghalani imevisaidia vyama vya Msingi vya Ushirika(Amcos) na Chama Kikuu cha Ushirika(Sonamcu) kupata fedha za kujiendesha na Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kupata mapato.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa wilaya ya Namtumbo Emmanuel Gwao, ameipongeza Serikali kwa kusimamia uuzaji wa mazao ya wakulima kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Amesema, mfumo huo umewaangalia zaidi wakulima ili wapate tija na umesaidia kutoa ajira za muda kwa baadhi ya watu wakiwemo wachukuzi na hata kufufua baadhi ya vyama vya Msingi vya ushirika vilivyopoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
0 comments:
Post a Comment