1. Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda
akipokea zawadi ya kitabu cha Texas Hill Country kutoka kwa Mgeni wake Balozi
wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright; Kitabu cha Texas Hill Country kinaelezea
taarifa mbalimbali kuhusu utalii na mambo mbalimbali kuhusu Jimbo la Texas.
1. Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda
akimsikiliza Mgeni wake Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright Ofisini
kwake Jengo la Kilimo IV Jijini Dodoma katika mazungumzo hayo Waziri Mkenda
amemueleza Mgeni wake kuwa Tanzania bado
inahitaji Wawekezaji zaidi kwenye Sekta ya Kilimo hususan kwenye mazao
ya mbegu za mafuta pamoja na mazao ya mboga na matunda (Horticultural Crops).
1. Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda
akimkabidhi Mgeni wake Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright zawadi ya
korosho za Tanzania mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisini
kwake Jengo la Kilimo IV Jijini Dodoma tarehe 16 Juni, 2021.
Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amemueleza Balozi wa Marekani
nchini Tanzania Dkt. Donald Wright kuwa Wakulima wa Tanzania wanahitaji uhakika
wa masoko ya mazao ya kilimo pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika na
kuongeza thamani mazao ya kilimo kutoka kwa Wawekezaji wa nchini Marekani na
kwamba Wizara ipo tayari kuratibu mkutano na Wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka
Marekani ili waje nchini kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo.
Waziri Mkenda amemueleza hayo Balozi Dkt. Wright tarehe 16 Juni
ofisini kwake Jijini Dodoma kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya
juhudi za makusudi kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakuwa chenye tija zaidi na
cha kumuinua Mkulima.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa bajeti ya Sekta ya Kilimo kwenye eneo
la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti imeongezeka mara dufu ili kuongeza
uzalishaji wa alizeti kama njia mojawapo ya kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka
nje ya nchi ambapo taifa hutumia zaidi ya shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta
ya kula kutoka nje ya nchi.
Waziri Mkenda amesema kuwa Wizara ya Kilimo imeweka mikakati
mbalimbali ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye mazao ya mafuta. Mikakati hiyo
ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mazao ya mafuta.
“Katika mwaka 2021/2022 Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya
Utafiti Tanzania (TARI) kutoka shilingi bilioni 7 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi
bilioni 11 mwaka 2021/2022 sambamba na hilo bajeti ya Wakala wa Mbegu wa Kilimo
(ASA) imeongezeka kutoka bilioni 5 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 10
mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za mazao
ya mafuta.” Amekaririwa Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda ameutaja mkakati mwengine ni pamoja na kuimarisha
huduma za ugani; ambapo Wizara itaendelea kuimarisha huduma za ugani kwa
kuwapatia vyombo ya usafiri maafisa ugani ikiwemo kununua pikipiki 1,500, vifaa
maalum vya kupimia udongo (Soil Test Kits), visanduku vya ugani (Extension
Kits), simu janja na kuwezesha uanzishaji wa mashamba ya mfano kwa kila afisa
ugani na kutoa mafunzo rejea.
“Huduma hizo zitawezeshwa kwa kuwa Wizara imeongeza bajeti ya
Kuimairisha huduma za ugani kutoka Shilingi milioni 603 mwaka 2020/2021 hadi
Shilingi bilioni 11 mwaka 2021/2022. Katika utekelezaji wa mpango huo, Wizara
imechagua Mikoa mitatu ya kielelezo; Mikoa hiyo ni Singida, Dodoma na Simiyu
yenye fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususan alizeti na pamba.”
Amekaririwa Prof. Mkenda.
Mkakati mwengine ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji wa mashamba
ya pamoja na kuimarisha kilimo cha mkataba.
“Wizara itaendelea kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya pamoja (block farming) katika mikoa inayozalisha mazao ya mafuta kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo mbegu bora, mbolea, viuatilifu na zana bora za kilimo pamoja na mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima.”
“Aidha, Serikali itaimarisha kilimo cha mkataba kwa mazao ya
mafuta kwa lengo la kuwa na uhakika wa masoko”. Alisisitiza Waziri Mkenda.
Kwa upande Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright amesema
Marekani na Tazania zinauhusiano mzuri na wa muda mrefu na kwamba itaendelea
kushirikiana na Tanzaniua katika Sekta ya Kilimo Mazao na kuahidi kuwa ubalozi
utatoa msaada kwa kila hitaji litakalokuwa ndani ya uwezo wa Taifa lake.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment