Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC ) kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja ya kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na Uvuvi ikiwa ni pamoja na mambo mengine ya kupambana na nzige.
Kadhalika Mawaziri hao wamejadili na kuweka mikakati ya kuchochea na kuongeza biashara ya mazao na mifugo kwa kupitisha itifaki inayotoa mwelekeo wa namna ya kukagua usalama wa chakula.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa utekelezaji wa mikakati ya bara la Afrika katika sekta hizo na kuona kiasi kilimo kinachangia maendeleo ya uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tanzania ni nchi yenye maslahi makubwa katika mkutano huu kwakuwa ni kapu la chakula katika nchi za Afrika Mashariki hivyo ni sehemu yetu nzuri ya kujenga mazingira ya biashara” Amesema Waziri Mkenda
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimekubaliana kwa kauli moja kuwa na ufuatiliaji na tathmini kwa mambo yote ambayo mikutano kama hiyo imekuwa ikikubaliana.
Waziri Mkenda amesema kuwa mkutano huo umejadili pia kuhusu upatikanaji wa mbolea kwa urahisi kwa wakulima ambapo sera maalumu imewasilishwa kwa ajili ya mapitio kwa nchi hizo zote ili kuwa na juhudi za pamoja ambazo zitapelekea kuweza kupata mbolea kwa bei rahisi katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Kuhusu swala la Sumukuvu, Waziri Mkenda amesema kuwa Tanzania na nchi zingine zitaendelea kufuata itifaki za Afrika Mashariki kwani kuna kiwango ambacho kimewekwa na jumuiya hiyo ambacho kinavumilika.
“Hatutaki sisi tumuuzie mtu chakula ambacho kina madhara na kwa bahati nzuri vipimo vinafanyika mipakani na karibia asilimia 99.9999% ya mahindi yanapopimwa yapo vizuri na haya mengine ambayo tunakuta yana utata kidogo ni matatizo ya vipimo, kwa hiyo itifaki ya namna ya kushughulikia swala la sumu kuvu ilikuwepo katika jumuiya ya Afrika Mashariki na tuna wajibu wa kuitekeleza” Amekaririwa Prof Mkenda
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Tanzania inalijali swala la Sumukuvu sio kwa sababu serikali inataka kuuza mazao nje bali ni kwa usalama wa wananchi watanzania na nje ya nchi ndio maana kuna mradi mkubwa kuliko nchi yoyote Afrika kwa ajili yakuhakikisha Sumukuvu inaendelea kupunguzwa katika mazao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment