METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, May 13, 2021

MRAJIS TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA AKALIA KUTI KAVU//WAZIRI MKENDA AAGIZA AJITATHMINI

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma, tarehe 13 Mei 2021 (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma, tarehe 13 Mei 2021. Mwingine pichani ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Andrew Massawe. 

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma, tarehe 13 Mei 2021, Mwingine Pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege ameagizwa kumsimamisha kazi Kaimu Mrajis Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Lindi Ndg Edmund Masawe.


Edmund amesimamishwa kazi kutokana na kukilazimisha Chama cha Ushirika wa mazao (AMCOS) cha Umoja kilichopo Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kukodi ghala kwa ajili ya kuhifadhia Korosho ilihali chama hicho kina ghala lake la kuhifadhia korosho.


Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ametoa agizo hilo tarehe 13 Mei 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Dodoma.


Mhe Mkenda amemtaka Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege kujitathmini kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi ya kutoa ushauri wake alioelekezwa wakati wa kikao cha majadiliano kilichofanyika tarehe 8 Mei 2021.


Waziri Mkenda amebainisha kuwa katika kikao kazi hicho Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini aliagizwa kutoa taarifa ya ushauri wake kuhusu Mradi wa pamoja wa vyama 32 vya msingi vya Ushirika (G32) vya Mkoani kilimanjaro lakini hakufanya hivyo.


“Katibu Mkuu Mimi nadhani Mrajis wa Vyama vya Ushirika anafanya mzaha, Anadhani siwezi kumng’oa na pengine mahali pa kuanza kupafumua katika Wizara ya Kilimo ni Tume ya Maendeleo ya Ushirika” Amekaririwa Mhe Mkenda


Prof Mkenda amesema kuwa amemuweka Mrajis na mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya ushirika katika uangalizi maalumu huku akimuagiza kufika Jumatatu tarehe 17 Mei 2021 kuwasilisha mapendekezo hayo haraka iwezekanavyo.


Waziri Mkenda amesema kuwa amekabidhiwa kuingoza Wizara ya Kilimo ili kuimarisha sekta ya Ushirika nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.


Akizungumzia kuhusu kadhia iliyoikumba Tanzania Kuhusu Nzige wa Jangwani amesema kuwa kati ya tarehe 14 Januari, 2021 na 24 Februari, 2020 Tanzania ilipata uvamizi wa Nzige wa Jangwa waliotokea nchi jirani ya Kenya na kuingia katika Wilaya nane (8) za Mwanga, Siha na Moshi (Kilimanjaro), Simanjiro (Manyara); Longido, Monduli na Ngorongoro (Arusha); na Lushoto (Tanga). Kati ya Wiaya hizo, nzige walikuwa wakihama kutoka kwenye maeneo waliokuingia na kulala maeneo mbalimbali ya Wilaya nne (4) Siha (Kilimanjaro), Simanjiro (Manyara); Longido na Monduli (Arusha) wakitanda kwenye eneo la jumla ya hekta 6,441.


Hata hivyo amesema kuwa serikali katika kukabiliana na kadhia hiyo imefanya juhudi kubwa ambapo iliunda timu za Viongozi na wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na viongozi wa Mikoa, Wilaya, vijiji na wananchi katika maeneo yaliyoripotiwa pamoja na Kufanya uchunguzi wa mahali nzige walipo, kutambua hatua zao za ukuaji na kuwadhibiti.


Kadhalika, juhudi zingine ni Kunyunyuzia kiuatilifu maalum aina ya Fenitrothion kwa kutumia ndege tatu (4) na Helkopta moja (1) kudhibiti makundi makubwa ya nzige wa jangwa na pia kwa kutumia vinyunyuzi (motorized sprayers) kwenye makundi madogo ya nzige pamoja na Timu za wataalam kwa kushirikiana na wananchi kufanya uchunguzi kwenye maeneo yote ambayo nzige walidhibitiwa ili kubaini endapo waliangua mayai na kudhibiti tunutu waliozaliwa.


MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com