Na Mathias Canal, WazoHuru
SERIKALI imewahakikishia wabunge kuwa imeweka mikakati ya kuhakikisha matumizi ya internet kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Andrea Kundo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (Chadema) aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya internet ili watanzania washiriki dunia ya TEHAMA na kidijitali.
Akijibu swali hilo, Kundo amesema kuwa asilimia kubwa ya watanzania hawatumii data na kuwa kwa sasa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha internet kwa Wananchi na kuwa mkakati uliopo Ni kuhakikisha matumizi ya internet yanaongezeka hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 43 ya sasa.
Aidha, katika swali la msingi la Mbunge wa Igalula, Daud Venant (CCM) aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupeleka mawasiliano ya simu kwenye vijiji vya Igalula ambavyo havina mawasiliano ya simu.
Akijibu swali hilo, Kundo amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ambapo mpaka sasa jumla ya kata 686 zimekwishafikishiwa huduma za mawasiliano nchi nzima na ujenzi wa minara ya mawasiliano unaendelea katika kata nyingine 371.
“Jimbo la Igalula lina Kata 11 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi 6 ya mawasiliano katika Jimbo la Igalula ambapo imejengwa minara 6 inayotoa huduma za mawasiliano katika Kata tano ambazo ni Kizengi, Loya (Miradi 2), Lutende, Miswaki na Tura”
“Kata zenye watoa huduma za mawasiliano katika Jimbo la Igalula ni 10 ambazo ni Igalula; Kigwa; Loya; Lutende; Miswaki; Kizengi; Miyenze; Tura; Goweko; na Nsololo.”
Kudo amesema pamoja na jitihada hizo za Serikali, Kata ya Mmale na baadhi ya maeneo ya kata za Jimbo la Igalula japo yana watoa huduma bado yanalalamikiwa kuwa yana changamoto za upatikanaji wa huduma za Mawasiliano.
Amesema Serikalii kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itavifanyia tathmini vijiji vyote vya Jimbo la Igalula.
“Vijiji vitakavyobainika kuwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za usoni kadri ya upatikanaji wa fedha” Amesema Naibu Waziri Kundo
MWISHO
0 comments:
Post a Comment