METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, June 9, 2019

Wachimbaji Madini Lindi watoa kilio Tume ya Madini

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa pili kushoto, Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma wa kwanza kushoto, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo mkoa wa Lindi Peter Ludovick mwenye suit ya Blue na Mhandisi kutoka tume ya Madini Fadhili Kitivai wakitoka kwenye machimbo ya madini ya Gypsum ya kampuni ya KNAUF Tanzania Ltd mkoani Lindi.
Faridu Sheweji mchimbaji mdogo wa madini ya Gypsum wilaya ya Kilwa akitoa maelezo kwa mwenyekiti na Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Kikula Katikati na Prof. Mruma wa kwanza kulia kuhusu shuguli zake alipotembelewa kwenye eneo lake la machimbo.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya KNAUF Tanzania Ltd Georgios Zachopoulos wa tatu kushoto akitoa maelezo kwa Mwenyekiti na Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa pili kushoto na Prof. Abdulkarim Mruma wa kwanza kushoto wakiwa kwenye eneo la machimbo. Wa tatu kulia ni Afisa Madini Mkazi mkoa wa Lindi Mhandisi Jeremiah Hango.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Kikula kushoto akikagua baadhi ya kifaa kinachotumika kufanyia tathmini ya thamani ya madini wakati wa mauzo ya madini kwenye soko la madini mkoa wa Mtwara lililopo kwenye jengo la Afisa Madini Mkazi Mtwara. Kushoto ni Kamishna wa tume hiyo Prof. Abdulkarim Mruma.
*****************************
Na Issa Mtuwa (Wizara ya Madini) Lindi na Mtwara Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amekutana na kilio cha wachimbaji wa madini mkoani Lindi kuhusu ongezeko la tozo zilizo kinyume cha sheria ya madini. Wakiongea kwa nyakati tofauti wachimbaji hao wamesema halmashauri za wilaya na vijiji zimekuwa zinawatoza tozo zaidi na ile iliyowekwa na sheria mama ambayo ni 0.03 badala yake wamekuwa wakitumia sheria ndogo (by law) zilizopitishwa na baraza la madiwani kuwatozo tozo zadi kinyume na sheria mama.
Wameongeza kuwa halmashauri zinatoza tozo zao, na halmashauri za vijiji nazo zinajipangia ushuru wao kitu ambacho kina kuwa kero na kusababisha usumbufu kilio ambacho walikiwasilisha wakati wa mkutano mkuu wa sekta ya madini uliofanyika tarehe 22/01/2019 chini ya uenyekiti wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Prof. Kikula amekutana na kilio hicho akiwa ziara mkoani humo kutembelea na kukagua shuguli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wadau wa madini. Kufuatia kilio hicho, Prof. Kikula ametoa wito kwa wachimbaji wa madini ya Gypsum, Kokoto, Chumvi na mchanga nchini kote kuwa na subira wakati Tume ya Madini ikihangaikia utatuzi wa changamoto hiyo ya utozwaji wa tozo zinazo tozwa na baadhi ya halmashauri za wilaya na vijiji kinyume na taratibu za sheria ya madini.
Prof. Kikula ameyasema hayo leo mara baada ya kutembelea machimbo mbalimbali ya madini ya Gypsum ikiwemo ya kampuni ya KNAUF Gypsum Tanzania Ltd, machimbo ya Mavuji yanayomilikiwa na mchimbaji mdogo Faridu Sheweji na mchimbo ya chumvi yanayomilikiwa na Magereza Lindi eneo la Machole.
Akijibu hoja ya kero hiyo, mwenyekiti wa tume amekiri uwepo wa malalamiko ya namna hiyo kutoka kwa wachimbaji wa mikoa mbalimbali nchini na siyo kwa Lindi peke yake. Anashangazwa na hali hiyo kwa kuwa sheria ya madini na miongozo mbalimbali iko wazi na inaelekeza vizuri kuhusu tozo zinazotakiwa kutozwa. Amesema wao kama tume wanafanya jitihada kutatua kero hiyo, hivyo watawasilisha malalamiko yao kwa mamlaka ya juu ambayo ni Waziri mwenye dhamana ya madini Doto Biteko ili aweze kuzungumza na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mita (TAMISEMI) Suleiman Jafo ili kuondoa kero hiyo.
“Nalitambua hili tatizo, kila tunapofanya ziara mikoa mbalimbali hii changamoto inajitokeza, sijui ni kwa nini inakuwa hivyo kwa sababu sheria iko wazi namna tozo zinavyotakiwa kutozwa. Naomba niwaahidi tutalishugulikia hili haraka sana, na mara baada ya ziara hii tutaandaa ripoti na kuiwasilisha kwa Waziri Biteko, pamoja na ripoti lakini pia nitamwambia kwa mdodomo ili kusisitiza juu ya kero hii” amesema Prof. Kikula.
Prof. Kikula ameziomba halmashauri na kila mdau wa madini kote nchini wazisome na kuzipitia vizuri sheria ya madini hususani inayohusu tozo mbalimbali za madini kabla ya kuanza kuwatoza wachimbaji. Mwenyekiti ameambatana na Kamishna wa Madini Prof. Abdulkarim Mruma walio anza ziara ya kikazi katika mikoa minne ya Lindi, Ruvuma, Njombe na Iringa katika kukagua shuguli za madini na kusikiliza na kutatua kero.
Wakati huo huo mwenyekiti wa Tume ya Madini amefanya mazungumzo na wafanyakazi wa Tume hiyo wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye ofisi za Afisa Madini Mkazi mkoa wa Mtwara. Amesikiliza kero za wafanyakazi hao hususani ukosefu wa watumishi na vitendea kazi. Kuhuusu magari amesema katika mwaka wa fedha ujao kila mkoa utapata gari jipya kuongezea yaliyopo na kuhusu watumishi suala hilo linafanyiwa kazi. Amewakumbusha kuhusu uadilifu katika kazi zao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com