Na Mathias Canal, Katavi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo amekipongeza kiwanda cha NGS kilichopo katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata Pamba kilichogharimu jumla ya Bilioni 4.5
Ametoa pongezi hizo leo Tarehe 2 Machi 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani humo kuanzia leo tarehe 2 Machi 2021 mpaka tarehe 3 Machi 2021 kwa ajili ya kujionea hali ya uwekezaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji.
Prof Mkumbo amesema kuwa muwekezaji wa kiwanda hicho ameitikia dhamira ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwekeza katika viwanda ikiwa ni muktadha wa kuimarisha ajira kwa wananchi.
“Nakupongeza sana Mhe Njalu kwa kuitikia mwito wa Rais Magufuli aliowataka wabunge nao kuwa wawekezaji lakini wewe umeanzisha kiwanda mapema kabisa na kuitikia mwito wa ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025” Amekaririwa Mhe Kitila
Ameahidi kuzungumza na waziri wa Nishati ili kuhakikisha kuwa changamoto ya ukosefu wa umeme katika mkoa wa Katavi inapatiwa ufumbuzi ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa upnde wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata Pamba NGS Investiment Co Ltd amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ulioanza Januari 2020 dhamira yake ni kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika Wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi.
Ameongeza kuwa dhamira ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi hususani wakulima kwani watalima huku wakijua soko lipo katika maeneo yao tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanalima pasina kujua muktadha wa soko.
Njalu amesema kuwa kiwanda kilipewa leseni/Kibali cha ununuzi wa Pamba msimu wa mwaka 2020/2021 kutoka Bodi ya Pamba Tanzania ambapo kwa msimu uliopita wa 2020/2021 kampuni yake iliweza kununua jumla ya Pamba Kilo 1,816,192 ambazo zina thamani ya fedha taslimu Shilingi 1,471,115,520 ambapo fedha hizo zote zimeshalipwa kwa wakulima.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha Robota 340 kwa siku yaani masaa 24 hivyo kwa mwezi mmoja uhitaji wa Pamba kwa ajili ya uzalishaji ni Tani 5,100 ambapo kwa msimu mzima kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha Tani 40,000 mpaka Tani 50,000
MWISHO
0 comments:
Post a Comment