METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 2, 2021

PROF MKUMBO ATEMBELEA ENEO MAALUMU LA UWEKEZAJI MKOANI KATAVI (HII NI AKILI KUBWA)

 

Waziri Nchi Ofisi ya Rais Prof. Kitila Mkumbo akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea na kukagua eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji Mkoani katavi.

Na Swaumu Katambo, Katavi

Waziri Nchi Ofisi ya Rais Prof. Kitila Mkumbo ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa Viwanda na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa kutoa eneo la uwekezaji wa kiwanda.

Pamoja na pongezi hizo Prof Mkumbo amesema kuwa Halmashauri kutoa eneo hilo ni "Akili kubwa" kwa kuwa wameangalia mbali kwani kitatoa fursa mbalimbali kwa wananchi zikiwemo ajira.

Ameyasema hayo leo tarehe 2 Machi 2021 wakati alipotembelea eneo hilo maalumu kwa ajili ya Viwanda wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Katavi.

Mkumbo amewasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa  wawekezaji kwenye mchakato mzima wa uwekezaji kwa kuwa ajira zikipatikana na Uchumi pia utapanda kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Juma Homera amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa kutenga eneo la uwekezaji ikiwa ni pamoja na wananchi kwa kukubali viwanda kijengwe katika Kata yao.

Pamoja na uwepo wa Changamoto ya Umeme utakaowezesha shughuli za ujenzi kukamilika kwa urahisi RC Homera amesema wamezungumza na watu wa Tanesco kuleta umeme katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuonesha kwa vitendo kuwa wanapokea wawekezaji Mkoani Katavi ili kuendelea kuzalisha ajira kwa wananchi pamoja na mzunguko wa pesa kuongezeka kwa ajili ya kukuza Uchumi.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com