METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, March 15, 2021

TATHMINI IFANYIKE MAENEO YOTE AMBAPO MINARA INAZIDIWA-MHANDISI KUNDO

 






Na Mathias Canal, Katavi

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Andrew Kundo (Mb) amewaomba wawekezaji na watoa Huduma za Mitandao ya mawasiliano kote Nchini kuhakikisha wanafanya tathmini ya mahitaji husika ya sasa katika maeneo ambayo minara inazidiwa.

Amewataka wawekezaji hao kuhakikisha kuwa wanayaboresha mawasiliano hayo, uwezo wake au kujenga minara mipya ili kuweza kusaidia katika maeneo husika.

Ameyasema hayo katika mwendelezo wa ziara zake za kukagua Miradi iliyopo chini ya Wizara ya Mawasilisiano na Taknolojia ya Habari akiwa katika eneo inapojengwa Bandari ya Karema iliyopo Mwambao wa Ziwa Tanganyika Mkoani Katavi ili kujionea uhalisia wa namna ya kuunganisha na kuimarisha mawasiliano katika ukanda wa ziwa Tanganyika.

Hata hivyo amewataka wawekezaji na watoa Huduma kuboresha maeneo ambayo yanatoa huduma ya mawasiliano ya simu pekee kuhakikisha wanaboresha huduma hiyo kutoka 2G hadi 3G ili watanzania wote waweze kutumia huduma ya Intaneti kwa kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025 inaelekeza kuhakikisha huduma ya Intaneti inapatikana kwa Asilimia 80%.

Mhandisi Kundo amesema serikali imejipanga kuangalia namna gani inavuta Mkonge wa Taifa kufika katika eneo la Bandari ya Karema ili kuhakikisha shughuli za Kitehama ikiwemo uwezo wa upatikanaji mtandao (Internet) kwa urahisi.

Kuhusu Changamoto ya Redio na Televisheni kutokuwa na usikivu wa kutosha katika maeneo ya Karema na Mishamo Naibu Waziri Mhandisi Kundo amesema wameshafanya mazungumzo na Shirika la Habari Tanzania (TBC) kuhakikisha kwamba uboreshaji wa Miundombinu ya TBC unarekebishwa ili kupata taarifa za kutosha na kuelimika kupitia Mawasiliano ya Redio.

Kadhalika, Naibu Waziri  Mhandisi Andrew Kundo (Mb) amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Juma Homera kwa usimamizi madhubuti wa kuimarisha masuala ya Ulinzi na Usalama ukilinganisha na miaka ya nyuma.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com