METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 2, 2021

SHERIA MPYA YA MADINI YAPELEKEA TANI 508.9 KUSAFIRISHWA NJE YA NCHI

 

Na Swaum Katambo-Katavi

Sheria mpya ya Madini ya uongezaji thamani madini chini ya kifungu cha 129 iloyopitishwa Agosti 28, 2020 inayoruhusu kusafirisha Makinikia nje ya Nchi yenye kiwango cha shaba kisichopungua asilimia 20 imesaidia kusafirisha Tani 508.9 za makinikia kutoka mgodi wa Katavi Mining Co.Ltd kwenda nje ya Nchi kwa mara ya kwanza.

Meneja wa Mgodi wa Katavi Mining Company Ltd Ndg Twalib Mohamed Seif ameyasema hayo leo tarehe 2 Machi 2021 wakati akitoa taarifa ya mgodi huo mbele ya Waziri Wa Nchi Ofisi Rais Uwekezaji Prof. Kitila Alexandra Mkumbo alipotembelea Kiwandani hapo na kubainisha kuwa jumla ya malipo yanayotokana na usafirishaji wa kwanza wa Makinikia ya Shaba ni kiasi cha Shilingi za kitanzania 449,251,452.22

Hata hivyo Twalib ameiomba Serikali iwapatie umeme wa uhakika ili kupunguza gharama za uzalishaji kwani kwa sasa wanatumia Jenereta kwa shughuli za uwezeshaji Mgodi.

Pia ameiomba Serikali kusaidia kutengeneza barabara yenye urefu wa Km 8 kutoka barabara kuu iendayo Sumbawanga hadi eneo la mgodi.

Kadhalika Seif ameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Madini Mpanda mkoani Katavi kuwapatia Mwongozo na usimamizi ili kuweza kufanikisha ununuzi wa Malighafi kutoka kwa wachimbaji wadogo.

Kuhusu barabara, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Juma Homera  amesema kuwa ili kutatua Changamoto hiyo serikali inaendelea kulifanyia kazi ambapo kwa ushirikiano na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) itatengenza.

Pia ameupongeza uongozi wa Katavi Mining Company Ltd kwani uwekezaji wao unaingizia Halmashauri kipato.

Kwa upande wake Waziri Wa Nchi Ofisi Rais Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameupongeza uongozi wa Katavi Mining Company Ltd kwa kufanya kazi nzuri huku akiitambua changamoto kubwa ya upatikanaji wa Umeme unaozikabili Kampuni za uwekezaji Mkoani Katavi hadi kupelekea kushindwa kufanya vizuri shughuli za uwekezaji.

Akizungumza na Mwekezaji wa Mgodi wa Katavi Mining Company Ltd Eng. Mahmoud Abdulrazack, Waziri Mkumbo amepongeza Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 na Kanuni zake na kusema kuwa baada ya Sheria hiyo wawekezaji wengi wa sekta ya Madini kutoka nchini Oman wamependezwa na uwekezaji nchini Tanzania.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com