SHULE ya sekondari ya Mbinga Girls ambayo inamilikiwa na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imeendelea kupata mafanikio makubwa kitaaluma tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014.
Mkuu wa shule hiyo
Efigenia Nzota amesema shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha nne
ilianzishwa kwa ajili ya wanafunzi wa kike ambapo ilianza kutoa wahitimu wa
kidato cha nne mwaka 2017 kwa kufaulisha kwa asilimia 95 ambapo kati ya
wahitimu 68 walifanya mtihani waliopata sifuri walikuwa watatu.
Nzota amesema mwaka
2018 jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne walikuwa 77 ambapo shule hiyo iliweza kufaulisha kwa
asilimia 98 na kwamba ni mwanafunzi mmoja tu ndiyo alipata daraja sifuri.
“Mwaka 2019 tulikuwa
na watahiniwa 108 ufaulu wetu ulikuwa kwa asilimia 100,matokeo haya ndiyo
yaliyotuwezesha kupata tuzo baada ya kuingia katika shule kumi bora kitaifa
katika kundi la shule za wananchi kwa kushika nafasi ya sita kati ya
kumi’’,alisema.
Kwa mujibu wa Mkuu
huyo wa shule,Mbinga Girls imeendelea kupata mafanikio makubwa kitaaluma ambapo
mwaka 2020,shule hiyo ilifaulisha kwa asilimia 100 kutokana na watahiniwa 93
kufanya mtihani na kufaulu wote.
Ameitaja siri kubwa
inayofanya shule hiyo kuendelea kufanya vizuri kitaalamu ni kila mwalimu
kutekeleza majukumu yake bila kusukumwa ambapo amesema kuna wakati walimu
wanafundisha hadi usiku na siku za Jumamosi na Jumapili.
Hata hivyo amesema
matokeo hayo mazuri ya mitihani yanatoa picha nzuri kwamba shule hiyo inakwenda vizuri kitaalum kwa sababu
imefanikiwa kuondoa sifuri na kiwango cha ufaulu kinaendelea kupanda mwaka hadi
mwaka.
“Matarajio yetu kama
walimu tunatamani ifike mahali katika shule hii division four isiwepo
kabisa,walau tuishie three,ili kufikia malengo yetu tunajenga mshikamano mkubwa
baina ya walimu na tunasisitiza maadili kwa wanafunzi wetu ili kuwaleta kwenye
ulimwengu wa kitaaluma’’,alisisitiza Nzota.
Ameutaja msingi
mkubwa katika shule hiyo ni kujenga nidhamu kwa wanafunzi ambapo tangu shule
hiyo imeanzishwa mwaka 2014 hadi 2021 jumla ya wanafunzi saba tu wameondolewa
kwa ujauzito.
Shule ya sekondari
Mbinga Girls ina walimu 19 na wanafunzi 453.
0 comments:
Post a Comment