METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, February 17, 2021

DKT. ABBASI: WASANII WAWEKEZE KWENYE KAZI BORA SIO KIKI

  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akijadiliana Jambo na Katibu wa kuratibu Serikali kuhamia Dodoma Bw. Meshack Bandawe, wakati akitembelea eneo la Kivukoni ambapo Serikali inakamilisha taratibu kuziweka katika ofisi moja taasisi za sanaa ambazo ni Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Taasisi ya Hakimiliki (Cosota) na Bodi ya Filamu Tanzania (FBT).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, ametoa msimamo kuwa Serikali haitapoteza muda na wasanii wanaoendeleza kiki badala ya kutumia muda wao vizuri kutengeneza kazi zao bora za sanaa.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo Dar es Salaam leo alipokuwa akitembelea eneo la Kivukoni ambapo Serikali inakamilisha taratibu kuziweka katika ofisi moja taasisi za sanaa ambazo ni Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Taasisi ya Hakimiliki (Cosota) na Bodi ya Filamu Tanzania (FBT).

“Serikali kama alivyoahidi Mhe Rais ipo kazini kuhakikisha sekta za sanaa zinakua na kuwapatia vijana mchango chanya. Hapa leo tunapambania taasisi zetu hizi muhimu kwa wasanii wapate ofisi nzuri na wawahudumie wasanii kutokea sehemu moja baada ya malalamiko ya miaka mingi kuwa ziko mbalimbali lakini unashangaa baadhi ya wasanii kuwaona siku mbili hizi wanaturudisha nyuma kwenye maisha ya kiki badala ya kazi bora,” alisema Dkt. Abbasi.

Aliongeza kuwa Serikali haitakuwa upande wa wasanii wanaovunja sheria za nchi na taratibu za kimaadili kwa manufaa yao binafsi badala yake itafanyakazi na wasanii wanaozidi kujielewa na wanaojua sanaa ya Tanzania iko wapi inatakiwa kwenda wapi.

“Jana nimeletewa habari nyingi sana, wengine wamepelekana polisi, wengine unasikia hivi, hawa wanaotaka kuturudisha nyuma Serikali hii haiwezi kuwaendekeza hao. Nawaongeza wasanii wote wawe wa muziki au filamu na sanaa nyingine wanaoendelea kupambana na kutoa kazi bora zinazoendelea kuiheshimisha sanaa yetu. Nasisitiza hizi ni zama za kazi sio kiki, waambieni hao vijana, wafikishieni ujumbe huu, anayesikia na asikie, hii ni sauti na amri kutoka Serikali Kuu,” alisema Dkt. Abbasi ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia ziara hiyo ya kukamilisha taratibu za ofisi za pamoja kwa taasisi hizo, Dkt. Abbasi alisema uamuzi umeshapitishwa na sasa ni taasisi hizo kugawiwa na kuhamia eneo moja na kuanza kutoa huduma bora kwa wadau wao kutokea sehemu moja kwa jijini Dar es Salaam wakati mipango kama hiyo ikiendelea kwa makao makuu Dodoma.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com