METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 23, 2020

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA DARAJA LA TANZANITE

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Tanzanite, jijini Dar es Salaam.

Mhandisi wa Madaraja Lulu Dunia, akifafanua jambo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Tanzanite, jijini Dar es Salaam.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa daraja la Tanzanite wa daraja jipya la Tanzanite (Salander) jijini Dar es Salaam na kwamba ameridhishwa na kasi ya mradi huo.

 

Amekagua ujenzi wa mradi huo leo (Jumanne, Desemba 22, 2020). Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03 na upana mita 20.5 litagharimu  sh. bilioni 243.75 na linatarajiwa kukamilika Oktoba 14, 2021.

 

“Nimekagua mradi na ujenzi wake unaendelea vizuri, sina mashaka na viwango na naamini utakamilika kwa wakati. Watanzania wanasubiri kwa hamu waanze kupita katika daraja hili.”

 

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ushiriki wa Watanzania katika ujenzi wa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini kwa kuwa inachangia katika kuongeza wataalamu.

 

Ujenzi wa daraja hilo una lengo la kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambayo inatumiwa  na magari mengi yanayoingia na kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam.

 

Mkandarasi anayejenga mradi huo ni kampuni ya GS Engineering Corporation kutoka Korea Kusini na hadi Novemba 30, 2020 utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 60.8.

 

Awali, Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Christianus Ako alisema hesabu ya mwaka 2017 ilionesha kuwa kiasi cha magari yanayopita kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwa siku kuwa ni wastani wa magari 42,000.

 

Alisema hadi sasa mradi umeajiri jumla ya wafanyakazi 590, kati yao asilimia 92 ni Watanzania na asilimia nane tu ni wataalamu kutoka nje ya nchi.

 

Mhandisi Ako alisema mradi huo pia unaendelea kutoa mafunzo kwa wahandisi 24 wa Kitanzania kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (5), wahandisi wahitimu (12) na wanafunzi wa uhandisi kutoka vyuo vikuu (7). “Mafunzo haya yatawajengea uwezo na ujuzi utakaosaidia Taifa hapo baadae.”

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com