METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, December 21, 2020

SHERIA INARUHUSU MAJINA YA WENZA KUSAJILIWA KATIKA HATI YA UMILIKI ARDHI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema sheria inaruhusu kuandikwa majina yote mawili ya wenza katika hati za umiliki ardhi.

Lukuvi alisema hayo tarehe 19 Desemba 2020 wilayani Siha mkoa wa Kilimanjaro alipokwenda kumaliza mgogoro wa ardhi baina ya Watawa wa Shirika la Kanisa Katoliki na wananchi wa kitongoji cha Mlangoni kuhusu Shamba la Kirari.

Alisema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikisajili Hati nyingi zenye majina yote mawili ya wenza na wengine husajili na majina ya watoto wao.

Kwa mujibu wa Lukuvi, siyo kweli kwamba Hati lazima isajiliwe kwa jina moja tu la mke au mume bali wote wawili wanaruhusiwa kitu cha msingi wawe na sifa za kumilikishwa.

Lukuvi alisema, hiyo ni fursa kwa wanawake kushawishi waume zao  katika kutekeleza suala hilo kwa kuwa sheria iko wazi  na hakuna Afisa Ardhi atakaye hoji suala hilo. 

"Akina mama mna ushawishi mkubwa  washawishini waume zenu waandike majina mawili ili kuepuka mgogoro" alisema Lukuvi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, hata mtoto chini ya miaka 18 anaweza kusajiliwa katika hati kwa masharti kuandikwa pia jina la msimamizi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com